Ripoti yafichua: Saudia na UAE zilipanga kuivamia kijeshi Qatar
(last modified Thu, 02 Aug 2018 08:06:59 GMT )
Aug 02, 2018 08:06 UTC
  • Ripoti yafichua: Saudia na UAE zilipanga kuivamia kijeshi Qatar

Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) mwaka jana zilipanga kuishambulia na kuivamia kijeshi Qatar mwanzoni mwa mgogoro wa kidiplomasia uliosababisha kuwekewa mzingiro na vikwazo taifa hilo dogo la Ghuba ya Uajemi.

Ripoti iliyochapishwa na taasisi ya The Intrecept imefichua kuwa mpango huo ulioratibiwa na warithi wa tawala za kifalme za Saudia na Imarati ulikuwa ushirikishe askari wa vikosi vya nchi kavu vya jeshi la Saudi Arabia, ambapo askari hao, kwa msaada wa jeshi la Imarati, wangevamia ardhi ya Qatar hadi umbali wa kilomita 100 na kuuteka mji mkuu wa nchi hiyo Doha.

Kwa mujibu wa afisa mmoja wa intelijinsia wa Marekani, maafisa wa intelijinsia wa Qatar nchini Saudi Arabia walipata fununu za mpango huo katikati ya mwaka jana, na hatimaye miezi kadhaa baadaye mashirika ya intelijinsia ya Marekani na Uingereza yakathibitisha kuwepo kwa njama hiyo.

Ripoti hiyo aidha imeashiria kampeni inayoendelea kufanywa na Umoja wa Falme za Kiarabu ya kuichokoza Qatar ili kupata kisingizio cha kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya nchi hiyo.

Qatar imelalamika mara kadhaa kuhusu ukiukaji wa mipaka ya anga yake unaofanywa na ndege za Imarati, na hata mapema mwaka huu ikachukua hatua ya kuuandikia barua Umoja wa Mataifa juu ya suala hilo.

Aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson (kushoto) na waziri wa mambo ya ne wa Saudia Adel al-Jubeir

Kwa mujibu wa maafisa wawili wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, zilikuwa zimesalia wiki chache tu kabla ya mpango huo wa uvamizi wa kijeshi wa Saudia na Imarati dhidi ya Qatar kutekelezwa, lakini ukasimamishwa na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson.

Ripoti hiyo aidha imeongeza kuwa Tillerson alifanya mazungumzo mara kadhaa kwa njia ya simu na maafisa wa Saudia kuwasisitiza wasichukue hatua ya kijeshi dhidi ya Qatar. Vilevile alimhimiza Waziri wa Ulinzi wa Marekani Jim Mattis awafahamishe maafisa wenzake wa ulinzi wa Saudia kuhusu hatari za uvamizi kama huo.

Itakumbukwa kuwa tarehe 5 Juni 2017, Saudi Arabia iliongoza nchi nyingine za Kiarabu za Misri, Imarati na Bahrain kuiwekea vikwazo vya angani, baharini na ardhini nchi ndogo ya Qatar na kukata kabisa uhusiano wao wa kidiplomasia na Doha. 

Mnamo tarehe 23 Juni, nchi hizo nne ziliipatia Qatar orodha ya masharti 13 na kutangaza kuwa kurejeshwa tena uhusiano wa kawaida na nchi hiyo kutategemea utekelezwaji wa masharti yote hayo na serikali ya Doha.

Masharti muhimu zaidi ambayo Saudia na washirika wake waliishurutisha Qatar ni kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Iran na Hizbullah ya Lebanon, kuifunga stesheni ya televisheni ya Aljazeera na kuondoa kituo cha kijeshi cha Uturuki ndani ya ardhi ya Qatar. Serikali ya Doha imekataa kutekeleza masharti hayo.../

Tags