Ansarullah yalaani kufukuzwa balozi wa Canada nchini Saudia, yamkaribisha Yemen
Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen amelaani kitendo cha Saudi Arabia cha kumfukuza balozi wa Canada mjini Riyadh na kuitaka Ottawa kufungua ubalozi wake San'a, mji mkuu wa Yemen.
Televisheni ya al Alam imemnukuu Muhammad Ali al Houthi akiandika leo katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: "Tunaialika serikali ya Canada kufungua ubalozi wake nchini Yemen; San'a inaikaribisha kwa mikono miwili hatua hiyo."
Ameendelea kuandika: Kufungua Canada ubalozi wake mjini San'a yatakuwa ni majibu mazuri kwa hatua ya udhalilishaji iliyochukuliwa na Saudi Arabia ya kukata uhusiano wake na Canada na kumfukuza balozi wa nchi hiyo mjini Riyadh.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudia, mapema leo asubuhi imempa balozi wa Canada muda wa masaa 24 ahakikishe ameondoka nchini Saudi Arabia kama njia ya kulalamikia hatua ya serikali ya Canada ya kusema kuwa ina wasiwasi na hatua zilizochukuliwa nchini Saudia za kuwatia mbaroni wanaharakati wa asasi za kijamii na wapigania haki za wanawake.
Aidha Saudia imemrudisha nyumbani balozi wake aliyekuweko Canada na imekata uhusiano wake wote wa kibiashara na Ottawa kwa madai kuwa Canada inaingilia masuala ya ndani ya Saudi Arabia.
Utawala wa kiimla wa Saudi Arabia siku ya Jumanne uliwatia nguvuni wanaharakati wawili wa masuala ya kijamii na haki za wanawake, Samar Badawi na Nassima al-Sada kama sehemu ya kukandamiza uhuru wa kujieleza nchini humo.
Serikali ya Canada kwa upande wake imeelezea kusikitishwa na hatua hiyo, jambo ambalo limeikasirisha Saudi Arabia na kuamua kukata uhusiano wake wa kidiplomasia na Ottawa na kusimamisha ushirikiano wake wa kibiashara na nchi hiyo.