HAMAS: Shambulio dhidi ya wanamapambano wa Muqawama halitaachwa bila kujibiwa
Msemaji wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema shambulio la ndege za kivita za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza dhidi ya kituo cha brigedi za Izzuddin al-Qassam, tawi la kijeshi la harakati hiyo ambalo limesababisha kuuawa shahidi wanamapambano wawili wa Muqawama halitaachwa bila kujibiwa.
Fawzi Barhum amesisitiza kuwa wazayuni maghasibu ndio wanaobeba dhima ya mauaji ya kigaidi ya wanamapambano wa brigedi za Izzudddin al-Qassam huko Bait Lahya kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.
Amebainisha kuwa: Muqawama hautasalimu amri kwa mauaji ya kigaidi na mashambulio ya makombora na mabomu na kwamba kuwalenga wanamapambano wa Muqawama hakutaachwa bila kulipia gharama yake kwa sababu Muqawama wa Palestina unao uwezo wa kuwalenga wazayuni maghasibu.
Jumatatu mchana jeshi la utawala wa Kizayuni lilishambulia ngome moja ya Muqawama wa Palestina katika eneo la Bait Lahya kaskazini mwa Ukanda wa Gaza na kuwaua shahidi Ahmad Marjan na Abdulhafidh As-Silawi, wanamapambano wa brigedi za Izzuddin al-Qassam, tawi la kijeshi la Hamas mbali na kuwajeruhi watu wengine kadhaa.
Wakati huohuo mtunguaji wa Muqawama Palestina amemwangamiza askari mmoja wa kizayuni karibu na mpaka wa pamoja wa Ukanda wa Gaza na Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Shirika la intelijinsia la utawala haramu wa Israel limetangaza kuwa mashambulio ya utunguaji yamewalenga wanajeshi wa utawala katika Ukanda wa Gaza. Shirika hilo la intelijinsia la utawala wa Kizayuni limekiri kuwa mtunguaji huyo wa Kipalestina ni mahiri mno.../