Arab League yaitaka jamii ya kimataifa iisaidie Palestina
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imelaani kushtadi wimbi la mauaji na jinai za kutisha dhidi ya Wapalestina zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel, huku ikiitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kukabiliana na jinai hizo.
Sambamba na kulaani mauaji ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza Ijumaa iliyopita, Saeed Abu Ali, Naibu Katibu Mkuu wa Arab League anayeshughulikia masuala ya Palestina amesema ni jambo la kusikitisha namna Wapalestina wanavyoendelea kuuawa kikatili mbele ya kimya cha jamii ya kimataifa.
Kadhalika ametoa mwito wa kushtakiwa utawala huo haramu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na mauaji ya kimbari unayoyafanya kwa lengo la kuimaliza jamii ya Wapalestina.
Afisa huyo mwandamizi wa Arab League amesema wakati umefika kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kushughulikia mafaili meusi ya jinai za kutisha za Israel yaliyowasilishwa kwake na Wapalestina.
Wapalestina wasiopungua saba waliuliwa shahidi na wengine zaidi ya 250 kujeruhiwa katika Ijumaa ya 29 ya maandamano ya "Haki ya Kurejea" yaliyofanyika kwa kaulimbiu ya "Intifadha ya Quds" huko Ukanda wa Gaza, Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Taarifa ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imetolewa katika hali ambayo, baadhi ya nchi za Kiarabu ziko mbioni kufanya wa kawaida uhusiano wao na utawala pandikizi wa Israel, unaowatendea jinai Wapalestina.