Helikopta ya Israel yawashambulia Wapalestina wa Ukanda wa Gaza
Helikopta ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel imeshambulia maeneo ya kusini mwa Ukanda wa Gaza, kwa madai kuwa hujuma hiyo ni ya ulipizaji kisasi baada ya Wapalestina kuwavurumishia roketi.
Taarifa ya jeshi la Israel iliyotumwa kwenye ukurasa wake wa Twitter imedai kuwa mashambulizi hayo ya usiku wa kuamkia leo yamelenga vituo vya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas.
Hata hivyo hakuna taarifa iliyotolewa kutoka Gaza kuhusu athari za hujuma hiyo ya helikopta ya kijeshi ya utawala katili wa Israel.
Katika hatua nyingine, Wizara ya Afya ya Gaza imesema jeshi la utawala haramu wa Israel limemuua shahidi kijana wa Kipalestina kwa jina Karam Fayyad (26) katika maandamano ya haki ya kurejea yaliyofanyika jana Ijumaa, katika mji wa Khan Yunis kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Tangu tarehe 30 Machi mwaka huu hadi sasa, Ijumaa ya kila wiki, maelfu ya Wapalestina hushiriki kwenye maandamano ya haki ya kurejea ili kuonyesha upinzani wao kwa uvamizi na ukaliaji wa mabavu wa ardhi zao unaofanywa na Wazayuni pamoja na sera zao dhidi ya taifa la Palestina.
Askari wa Kizayuni wanawashambulia moja kwa moja kwa risasi moto waandamanaji hao wasio na ulinzi na kuwaua shahidi au kuwajeruhi kadhaa miongoni mwao.