Wanawake wafungwa wa kisiasa Saudi Arabia wakabiliwa na mateso makali
Wafungwa wa kisiasa waliopo jela nchini Saudi Arabia wanakabiliwa na mateso makali zaidi wanayofanyiwa kwa kutumia njia mbalimbali.
Tovuti ya habari la al Ahad imeripoti kuhusu namna wanawake wanaharakakati wa kisiasa na wa haki za binadamu waliofungwa jela nchini Saudia wanavyoteswa katika jela na korokoro mbalimbali nchini humo. Kwa mujibu wa tovuti hiyo ya habari, taasisi ya Kutetea Haki za Binadamu ya al Qist imetoa taarifa mpya kuhusu vitendo viovu wanavyofanyiwa wafungwa wa kisiasa katika jela nchini Saudi Arabia na kufichua kuwa: Wafungwa hao wanakabiliwa na mateso ya ukatili wa hali ya juu. Taarifa hiyo imeongeza kuwa baadhi ya mateso hayo wanafanyiwa wafungwa wa kisiasa wanawake chini ya usimamizi wa Saud al Qahtani aliyekuwa mshauri wa ofisi ya Mfalme wa Saudi Arabia na mmoja wa watu wa karibu na Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo.

Taasisi ya al Qist imeongeza kuwa: Wafungwa wa kisiasa kama Samar Badawi, Shadin al Anzi, Aziza Yusuf, Iman al Nafjan na Lajin al Hadhlul wanakabiliwa na mateso mbalimbali ikiwemo kuteswa kwa mshtusho wa umeme na hata kudhalilishwa wakati wakihojiwa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, alama na athari za kuteswa wafungwa hao zinaonekana usoni na kwenye miili yao huku wakiwa wamepungua sana uzito wa mwili. Mfungwa mmoja kati ya hao waliotajwa amenukuliwa akisema kuwa Saud al Qahtani mara kwa mara amekuwa akishuhudiwa katika chumba cha mateso. Al-Qahtani aidha aliwahi kumwambia mfungwa mmoja kuwa ataukata mwili wake vipande vipande na kuumiminia asidi na kisha kuutumbukiza kwenye shimo la maji taka.