Polisi wa Israel wawashambulia Wakristo waliopinga kudhalilishwa Nabii Issa (as)
Maandamano ya amani ya Wakristo wanaoishi ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) yamefanyika karibu na jumba la makumbusho la mji wa Haifa wakipinga picha za kumvunjiwa heshima Nabii Issa (Yesu Kristo) ambapo yameishia kwenye ghasia na machafuko baada ya kushambuliwa na polisi wa utawala haramu wa Israel.
Wakristo wanaoishi Israel waliokuwa wakipiga nara za kupinga kitendo cha kudhalilishwa na kuvunjiwa heshima Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu, wametaka kuondolewa masanamu na picha zote zinazomvunjia heshima Nabii Issa na mama yake, Bibi Maryam (as). Polisi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walivamia maandamano hayo ya amani kwa kutumia mabomu ya sauti na gesi ya kutoa machozi kwa lengo ya kuwatawanya waandamanaji.
Ripoti zinasema katika jumba hilo la makumbusho la mji wa Haifa kumewekwa picha na masanamu ya Bibi Maryam na Nabii Issa Masiih (as) inayofanana na vibonzo, suala ambalo limewakasirisha mno Wakristo wanaoishi ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).
Wakristo wa Kiarabu huko Israel wanaishi katika miji ya Nazareth, Haifa na Acre (Akko) na katika kijiji cha al Jalil (Galilee) na wanasumbulwia na ubaguzi wa hali ya juu wa kijamii, kiuchumi na kisiasa.