HAMAS yasisitizia kuundwa muungano wa nchi zinazoihami Palestina
Mahmoud Az-Zahar, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema, adui wa Lebanon, Syria na Gaza ni utawala ghasibu wa Kizayuni tu; na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni muungaji mkono wa wanamapambano wa muqawama.
Az-Zahar ameyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Palestina la Shahab na kuongeza kuwa: Palestina inapaswa iongeze kiwango cha uhusiano wake na Iran, Uturuki na nchi zote za Kiarabu na Kiislamu na kutekelezwa mpango unaoungwa mkono na Waarabu na Palestina yenyewe kwa ajili ya kuunga mkono na kufanikisha ukombozi wa Palestina.
Afisa huyo mwandamizi wa Hamas amesisitiza kuwa, harakati hiyo inataka kufikia mapatano, lakini kuna tofauti kati ya mpango wa mapatano unaoungwa mkono na makundi ya Palestina na mpango uliopo ambao una dhamira ya kuupigisha magoti muqawama.
Dakta Mahmoud Az-Zahar ameeleza pia kwamba, endapo Mahmoud Abbas atagombea urais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina atashindwa, kwa sababu amewatendea jinai wananchi wa Palestina; na bunge la Palestina halitampitisha kuwania nafasi hiyo.
Katika mahojiano aliyofanya siku ya Jumatano na gazeti la Falastin-Alyaum, Az-Zahar alisema, kwa kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umezivamia na kuzikalia kwa mabavu sehemu za ardhi za Lebanon, Syria na Palestina, kuna udharura wa kuwepo uratibu na mashauriano baina ya mihimili hiyo mitatu ya muqawama kwa ajili ya kupambana na utawala huo ghasibu.../