HAMAS yakaribisha kufanyika uchaguzi mkuu wa Palestina katika ngazi zote
Mjumbe mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitizia kufanyika uchaguzi wa Palestina katika ngazi zote ukiwemo wa Bunge, Rais wa Mamlaka ya Ndani na Baraza la Taifa.
Ismail Ridhwan ameuambia mtandao wa habari wa Ar-Risalah Net kwamba, uchaguzi huo wa ngazi zote inapasa ufanyike kulingana na makubaliano ya Cairo na Beirut; na uongozi wa Mamlaka ya Ndani ulioko Ramallah unapaswa kuliheshimu suala hilo.
Kiongozi huyo mwandamizi wa Hamas amesisitiza pia kwamba, maandamano ya Haki ya Kurejea wakimbizi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza na ardhi zilizoanza kukaliwa kwa mabavu mwaka 1948 yataendelea hadi yafikiwe malengo yaliyokusudiwa.
Maandamano ya Haki ya Kurejea yalianza tarehe 30 Machi mwaka 2018 kwa lengo la kuhitimisha ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na utawala ghasibu wa Kizayuni na kuuvunja mzingiro dhidi ya Ukanda wa Gaza. Hadi sasa Wapalestina zaidi ya 250 wameuliwa shahidi katika maandamano hayo kwa kupigwa risasi na askari wa utawala haramu wa Israel na wengine wasiopungua elfu 36 wamejeruhiwa.
Ismail Ridhwan vile vile ameuonya utawala wa Kizayuni kuhusiana na kuendeleza kwake uchokozi na jinai dhidi ya wananchi wa Palestina na kubainisha kwamba: Mhimili wa muqawama utatoa jibu kali na imara dhidi ya uchokozi huo.../