Harakati ya Hamas yakosoa siasa za Rais Mahmoud Abbas
(last modified Tue, 26 Feb 2019 02:38:24 GMT )
Feb 26, 2019 02:38 UTC
  • Harakati ya Hamas yakosoa siasa za Rais Mahmoud Abbas

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina anakubaliana na mpango wa Marekani wa "Muamala wa Karne" lakini viongozi wa Fat'h wanataka kumuonyesha kiongozi huyo kwamba, anaupinga mpango huo.

Abdul-Latif al-Qanui amebainisha kwamba, lengo la Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ni kutekeleza mpango wa Marekani wa "Muamala wa Karne" na badala ya kuwaunganisha Wapalestina, Mahmoud Abbas amekuwa akifikiria kuleta mifarakano na migawanyiko miongoni mwa Wapalestina.

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS  amesema bayana kwamba, hatua za Mahmoud Abbas za kuwaadhibu wananchi wa Gaza, njama zake za kutaka kujitenga na hatua zake za chuki na hasama dhidi ya makundi ya mapambano ya Palestina ni ishara ya wazi ya kuwa pamoja kiongozi huyo na adui Mzayuni.

Maandamano ya kupinga mpango wa Marekami wa "Muamala wa Karne"

Kwa mujibu wa mpango wa Marekani wa "Mumala wa Karne", mji wa Quds utakabidhiwa kwa Israel, wakimbizi wa Kipalestina hawatakuwa na haki ya kurejea kwao, utawala haramu wa Israel utasimamia usalama wa sehemu kubwa ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na vivuko vya mpakani huku maeneo pekee ya Kiarabu ya Quds Mashariki yakiunganishwa na nchi ya Palestina.

Kadhalika kwa mujibu wa mpango huo eneo la Ukanda wa Gaza litaunganishwa na nchi mpya ya Palestina kwa sharti la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu Palestina HAMAS kukubali kuweka chini silaha. Katika hatua  mpya zinazochukuliwa na Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina dhidi ya Wapalestina, kiongozi huyo ameondoa wafanyakazi wa mamlaka hiyo katika kivuko cha mpakani cha Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Tags