Hizbullah: Muqawama ni tishio kubwa kwa adui Mzayuni
Mkuu wa Baraza la Utendaji la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, nguvu na uwezo wa muqawama ni tishio kubwa kwa adui Mzayuni.
Shirika la habari la IRIB limemnukuu Sheikh Ali Damush akisema hayo katika eneo la Ras al Nabi'i mjini Beirut na kuongeza kuwa, Lebanon ndiyo medani kuu ya mapambano ya muqawama dhidi ya Marekani na waitifaki wake.
Sheikh Damush amesisitiza kuwa, maadamu Marekani na waitifaki wake wanaendelea kutishia usalama wa Lebanon, na madhali wanaendelea kutoa vitisho vya vikwazo na mashinikizo, basi watambue kuwa muqawama nao utaendelea kuwa tishio kwao.
Mkuu huyo wa Baraza la Utendaji la Hizbullah ya Lebanon ameongeza kuwa, umoja na mshikamano wa kitaifa wa wananchi wa Lebanon utavunja njama na fitna zote za Wamarekani na kwamba kamwe muqawama hautoathiriwa na uchochezo na maneno ya uongo ya viongozi wa Marekani.
Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Hizbullah ya Lebanon aidha amesisitiza kuwa, umoja wa kitaifa, muqawama na utayari wa wananchi ndilo sharti la kuweza kulindwa usalama wa Lebanon mbele ya tamaa na vitisho vya Israel.
Amesisitiza pia kuwa, wananchi wa Lebanon wanapaswa kuwa macho na makini sana mbele ya njama za maadui wa taifa lao.