Kesho Jumanne, Siku ya Kwanza Ramadhani Iraq, Iran, Oman
Kesho Jumanne Mei 7 itasadifiana na siku ya kwanza ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani katika nchi kadhaa duniani.
Nchini Iraq, Ofisi ya Ayatullah Sayyid Ali Sistani, Marjaa mkuu wa kidini imetangaza kuwa kesho Jumanne itakuwa siku ya kwanza ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Taarifa ya Ofisi ya Sistani imesema: "Kwa kuzingatia kuwa haijathibiti kuandama mwezi Jumapili, usiku, leo Jumatatu itakuwa siku ya mwisho ya Mwezi wa Shaaban na kesho Jumanne (Mei Saba) itakuwa siku ya kwanza ya Mwezi Mmtukufu wa Ramadhani mwaka 1440 Hijria Qamaria.
Baadhi ya nchi za Kiislamu kama vile Kuwait, Bahrain, Imarati, Qatar, Lebanon, Libya, na Afghanistan zimetangaza leo kuwa siku ya kwanza ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Nchini Tanzania, Kadhi Mkuu Abdallah Mnyasi naye pia ametangaza kuwa Jumanne ya Mei 7 ni siku ya kwanza ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani akifafanua kuwa mwandamo wa mwezi haujaonekana. Lakini katika nchi jirani ya Kenya Kadhi Mkuu Sheikh Ahmed Muhdhar ametangaza leo kuwa siku ya kwanza ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani nchini humo baada ya kusema kuwa jana jioni mwezi mwandamo ulishuhudiwa katika eneo la Hola, Kaunti ya Tana River.
Katika nchi kama vile Oman, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan kesho Jumanne ni siku ya kwanza ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani baada ya mwezi mwandamo kutoonekana katika nchi hizo. Aidha Waislamu wa nchi za China, Australia na New Zealand nao pia wametangaza kuwa kesho Jumanne ni siku ya kwanza ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran inawaombea Waislamu wote kheri za mwezi huo mtukufu ambao ni hiba, atia na zawadi kubwa sana inayotoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waja wake anaowapenda.