Milipuko kadhaa mikubwa katika Bandari ya al-Fujairah UAE
Milipuko kadhaa mikubwa imeripotiwa kujiri katika Bandari ya al-Fujairah katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Kwa mujibu wa Televisheni ya Al Mayadeen, milipuko hiyo imejiri mapema Jumapili asubuhi katika bandari muhimu ya al-Fujairah ambapo meli kadhaa za kubeba mafuta zinaripotiwa kuteketea moto.
Mashuhuda wanasema punde baada ya milipuko hiyo, ndege za kivita za Marekani na Ufaransa zimeonekana zikiruka juu ya bandari hiyo.
Bado haijajulikana chanzo cha milipuko hiyo iliyojiri katika bandari ya Al Fujairah ambayo hutumika kusafirisha mafuta ghafi ya petroli na bidhaa zinginezo.

Taarifa zinasema meli za kubeba mafuta ghafi ya petroli ambazo zimeteketea moto kufuatia milipuko hiyo ya Al Fujairah ni pamoja na Al Majd, Nambari 9773800, Al Marzouq Nambari 9165762, Al Marij Nambari 9394741, Al Amijal Nambari 9147764 na Khamsa 10, Nambari 94320704.
UAE imejenga bomba la mafuta lenye urefu wa kilomita 370 kutoka Abu Dhabi hadi Bandari ya Al Fujairah iliyo katika Bahari ya Oman ili kwa mtazamo wao, wakwepe kutumia Lango Bahari la Hormoz.