Wairaq wafanya maandamano makubwa kulaani siasa za Marekani dhidi ya Iran
Maelfu ya raia wa Iraq wamefanya maandamano makubwa katika miji mbalimbali ya nchi hiyo ukiwemo mkoa wa Baghdad na Basra wakilalamikia siasa za uhasama za Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Washiriki wa maandamano hayo sambamba na kupiga naraza kulaani siasa mbovu za uhasama wa Marekani dhidi ya Iran na eneo la Asia Magharibi, wamewataka wawakilishi wa bunge la Iraq kupitisha muswada ambao utawaondoa askari wa Marekani kutoka ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu. Aidha Wairaqi katika maandamano hayo wamesisitiza kwamba hawataki kushuhudia hata kidogo vita dhidi ya nchi jirani na Iraq. Kabla ya hapo pia wafuasi wa Sayyid Muqtada al-Sadr, Kiongozi wa Harakati ya Sadr nchini Iraq walifanya maandamano mjini Karbala na Baghdad wakionyesha upinzani wao kwa hatua za Marekani za kutaka kuanzisha vita katika eneo la Asia Magharibi na kutaka kuiingiza nchi yao katika vita hivyo.
Itakumbukwa kuwa Jumatatu iliyopita, Rais Donald Trump wa Marekani na katika mwendelezo wa hatua zake za uhasama dhidi ya Tehran, aliandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii ya Twitter wenye vitisho kuilenga Iran ya Kiislamu. Habari zinasema kuwa Trump anakusudia kutuma askari zaidi 1500 katika eneo la Asia Magharibi, kama ambavyo kanali ya televisheni ya CNN imetangaza kwamba rais huyo amekubali mpango wa kutumwa zana za kijeshi na askari zaidi katika eneo hili.