Ban asema Israel inavuruga mpango wa amani
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amekosoa vikali hatua ya Israel kuendeleza ujenzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Akizungumza mbele ya Baraza la Usalama, Ban amesema, hatua hizo za Israel kupora ardhi ni kizingiti katika jitihada za kupatikana amani Palestina.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia amebainisha wasiwasi wake kuhusu Israel kuendelea kubomoa nyumba za Wapalestina na kusema mazingira yanayotawala sasa yametatiza juhudi za kupatikana amani.
Amesema kubomolewa nyumba za Wapalestina na kujengwa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ni mambo yanayoibua swali kuhusu iwapo lengo la Israel ni kuwatimua Wapalestina kutoka maeneo kadhaa ya Ukingo wa Magharibi na hatimaye kuzuia kuundwa taifa huru la Palestina.
Tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka uliopita wa 2015 hadi sasa maeneo mbalimbali ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu yamekuwa yakishuhudia wimbi la malalamiko ya upinzani dhidi ya siasa za kichokozi za utawala wa Kizayuni na njama za utawala huo za kuvuruga utambulisho wa Baitul Muqaddas pamoja na mpango wake wa kuugawa kiwakati na kimahali msikiti mtukufu wa Al-Aqsa. Wimbi hilo la malalamiko limekuwa maarufu kwa jina la Intifadha ya Quds.
Wapalestina zaidi 210 wameshauawa shahidi tangu ilipoanza Intifadha ya Quds mwezi Oktoba mwaka jana hadi hivi sasa.