Hamas: Trump hawezi kuwatenganisha Wapalestina na Quds Tukufu
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imesema mpango wa Rais Donald Trump wa Marekani wa muamala wa karne hauwezi kuwapokonya Wapalestina mji wa Quds (Jeruusalem) ambao unakaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Akizungumza katika Ukanda wa Ghaza, kiongozi wa Hamas Ismail Haniya amesema Quds Tukufu haiwezi kugawanya kwa pande za mashariki na magharibi kwani mji wote huo ni wa Kiislamu na ni milki ya Wapalestina wote.
Ameongeza kuwa, Trump na njama zake dhidi ya Wapalestina haziwezi kubadilisha utambulisho wa mji mtakatifu wa Quds ambao unakaliwa kwa mabavu na Israel. Haniya amesema mpango wa rais wa Marekani wa eti 'Muamala wa Karne' hauwezi kuwapokonya Wapalestina Quds Tukufu na msikiti wa Al Aqsa ulio mjini humo.
Haniya amebainisha wazi kuwa, "Mji wa Quds hauna mashariki wala magharibi bali wote ni wa Kiislamu na Trump, utawala wa Marekani, muungano wa Kizayuni-Marekani, kimya cha kimataifa na njama za kuwa na uhusiano wa jawaida na utawala wa Kizayuni au kuhamishia ubalozi katika mji wa Quds, yote hayo hayawezi kubadilisha uhalisia wa mambo."
Ikumbukwe kuwa Disemba mwaka 2017, Trump aliutambua mji wa Quds kuwa eti ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel na kutangaza kuuhamishia ubalozi wa Marekani katika mji huo.
Aidha hivi karibuni kumevuja mpango wa 'Muamala wa Karne' wa Rais Trump wa Marekani wenye lengo la kukandamiza kabisa haki za taifa la Palestina kwa maslahi ya utawala haramu wa Israel.