Wapalestina 79 wajeruhiwa katika maandamano ya 'Haki ya Kurejea'
Wizara ya Afya ya Palestina imesema Wapalestina 79 wamejeruhiwa katika Ijumaa ya 63 ya maandamano makubwa ya 'Haki ya Kurejea' katika Ukanda wa Ghaza.
Kwa mujibu wa taarifa, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walifyatua risasi za vita na kutumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya Wapalestina ambao walikuwa wakiandamana kwa amani.
Maandamano ya 'Haki ya Kurejea' ya Ijumaa hii yalifanyika chini ya nara na kaulimbiu ya 'ardhi yetu ya jadi haiuzwi.'
Tangu tarehe 30 Machi mwaka 2018 hadi hivi sasa, Wapalestina 310 wameshauawa shahidi kwa kupigwa risasi na wanajeshi katili wa Israel na zaidi ya 31 elfu wengine wameshajeruhiwa.
Nchi nyingi duniani ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na mashirika mbalimbali ya kimataifa, yamekuwa muda wote yakilaani jinai zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina.
Wimbi hili la maandamano ya Wapalestina ni la kukumbuka jinai nyingine ya utawala wa Kizayuni ya kuteka ardhi nyingine za Wapalestina tarehe 30 Machi 1976.
Siasa kuu za utawala wa Kizayuni wa Israel ni kuwapora Wapalestina ardhi zao na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwa shabaha ya kuvuruga muundo wa kijiografia wa maeneo ya Palestina na kuyapa maeneo hayo sura ya Kizayuni.