Ansarullah: Mkutano wa Bahrain ni uhaini dhidi ya Wapalestina
Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, mkutano wa Marekani uliofanyika siku chache zilizopita katika mji mkuu wa Bahrain, Manama kwa shabaha ya kuzindua Muamala wa Karne ni hujuma ya moja kwa moja na uhaini dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.
Abdul-Malik Badruddin al-Houthi alisema hayo katika hotuba ya jana Alkhamisi kwa njia ya televisheni mjini Sana'a na kubainisha kuwa, mkutano huo wa Juni 25 na 26 uliopewa anuani bandia ya 'Kuvutia Uwekezaji Palestina' ni uhaini wa kiwango cha juu kabisa dhidi ya Wapalestina.
Kiongozi huyo wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesisitiza kuwa, wananchi wa Yemen wataendelea kusimama bega kwa bega na wananchi wa Palestina katika jitihada na harakati zao za kupigania uhuru, ardhi na taifa lao.
Abdul-Malik Badruddin al-Houthi amesisitiza kuwa, mkutano huo ni sehemu ya kujidhalilisha na kujipendekeza utawala wa Aal-Saud wa Saudia Arabia kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Ameeleza bayana kuwa, haiwezekani kufanya uhusiano na adui Mzayuni na kwamba kufanya uhusiano na utawala huo ni kupuuza kadhia muhimu ya Umma wa Kiislamu ambayo ni kadhia ya Palestina.
Mpango huo wa Muamala wa Karne umekabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Wapalestina wenyewe na Waislamu kote duniani. Maandamano ya kupinga mpango huo yamefanyika katika nchi kadhaa duniani kama vile Morocco, Palestina na baadhi ya maeneo ya Bahrain. Wananchi wa Iraq usiku wa kuamkia jana walishambulia ubalozi wa Bahrain mjini Baghdad, kupinga kitendo hicho cha Manama kuwa mwenyeji wa njama na fitna hizo za Marekani na Wazayuni dhidi ya Wapalestina.