Palestina: Kikao cha Manama kinaashiria kufeli utawala wa Trump
Msemaji wa Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema mkutano wa Marekani uliofanyika siku chache zilizopita katika mji mkuu wa Bahrain, Manama kwa shabaha ya kuzindua Muamala wa Karne umeonesha ni jinsi gani sera na mipango batili ya utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani imefeli.
Nabil Abu Rudeineh alisema hayo jana Jumamosi na kusisitiza kwamba lengo la mpango wa Muamala wa Karne ni kuisambaratisha kabisa kadhia ya Palestina.
Ameeleza bayana kuwa, hatua ya Wapalestina ya kuususia mkutano huo wa Juni 25 na 26 uliopewa anuani bandia ya 'Kuvutia Uwekezaji Palestina' imetuma ujumbe mzito na wa wazi kwa utawala wa Trump.
Hii ni katika hali ambayo, Michael Lynk Ripota Maalumu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu amesema kuwa, mpango wa Kimarekani-Kizayuni wa "Muamala wa Karne" utashindwa na kugonga ukuta.
Amesisitiza kuwa, mpango wowote wa mapatano ukiwemo ule wa Muamala wa karne ambao hauoani na sheria na maazimio ya kimataifa utafeli na kushindwa.
Hapo jana Jumamosi pia, Meya wa mji wa Yatta, Ibrahim Abu Zahra aliibadilisha jina la barabara ya 'Bahrain' katika eneo la al-Khalil katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuiita “Marzouq al-Ghanim" jina la Spika wa Bunge la Kuwait ambaye amekuwa miongoni mwa viongozi wachache wa nchi za Kiarabu wanaoliuga mkono kwa dhati taifa huru la Palestina.