Mpango wa Muamala wa Karne, Palestina yakataa upatanishi wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i54562-mpango_wa_muamala_wa_karne_palestina_yakataa_upatanishi_wa_marekani
Wiki mbili tu baada ya mkutano wa utangulizi wa kutekeleza mpango uliopewa jina la "Muamala wa Karne" huko Manama nchini Bahrain, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa, Palestina haikubali upatanishi wa Marekani katika kadhia ya Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 05, 2019 02:36 UTC
  • Mpango wa Muamala wa Karne, Palestina yakataa upatanishi wa Marekani

Wiki mbili tu baada ya mkutano wa utangulizi wa kutekeleza mpango uliopewa jina la "Muamala wa Karne" huko Manama nchini Bahrain, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa, Palestina haikubali upatanishi wa Marekani katika kadhia ya Palestina.

Mahmoud Abbas amesisitiza kuwa, Marekani ambayo inatayarisha mazungumzo inapaswa kwanza kutambua rasmi njia ya utatuzi ya kuundwa nchi huru ya Palestina mji wake mkuu ukiwa Quds tukufu.    

Ripoti zinasema kuwa, mpango wa Kimarekani wa Muamala wa Karne umupuuza kabisa suala la kuundwa nchi huru ya Palestina. 

Quds ambacho ni kibla cha kwanza cha Waislamu ndio kadhia muhimu zaidi ya Umma wa Kiislamu, na Marekani inafanya jitihada za kufuta utambulisho wa Kiislamu na Kipalestina wa mji huo mtakatifu kwa kutambua rasmi kuwa ni eti mji mkuu wa utawala ghasibu wa Israel. Kuhusiana na suala hilo Hussein Ajirlo ambaye ni mtaalamu wa masuala ya magharibi mwa Asia anasema: "Kwa mujibu wa mpango wa Muamala wa Karne, Quds inatambuliwa kuwa ni mji mkuu wa Israel na kitongoji kimoja kidogo kilichoko kandokando ya mji huo kimepangwa kuwa mji mkuu wa Palestina." 

Mpango huo wa Donald Trump ambao umesukwa na kupikwa na mkwe wake Myahudi, Jared Kushner, hautambui haki yoyote ya wananchi wa Palestina. Miongoni mwa malengo makuu ya mpango huo wa Kimarekani ni kupinga katakata suala la kurejea wakimbizi wa Kipalestina katika ardhi ya jadi na ya mababu zao na badala yake kupewa makazi katika nchi nyingine kama Misri na Jordan na kupokonywa silaha makundi ya mapambano ya ukombozi ya Palestina. 

Hossein Amir-Abdollahian ambaye ni msaidizi wa Spika wa Bunge la Iran katika masuala ya kimataifa anasema: "Marekani inafanya njama za kuliondoa kabisa suala la wakimbizi wa Kipalestina katika ajenda ya mazungumzo. Kupitia njia ya kushauriana na washirika wake na kutoa vishawishi, Washington inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba, wakimbizi wa Palestina waliofukuzwa na Israel katika nchi yao wanapewa makazi katika nchi walikokimbilia." 

Hossein Amir-Abdollahian

Ni kwa kutilia maanani sura halisi ya mpango wa Muamala wa Karne na malengo yake ndiyo maana makundi na harakati mbalimbali za Palestina zikasusia mkutano wa kiuchumi wa Manama uliofanyika tarehe 25 hadi 26 za mwezi uliopita huko Bahrain. Makundi hayo yanasisitiza kuwa, mpango wowote wa amani ambao hautaitambua rasmi Quds kuwa ni mji mkuu wa daima wa Palestina na kutambua rasmi haki nyingine za kisheria za taifa hilo ikiwemo haki ya kurejea wakimbizi katika nchi yao, utafeli na kushindwa. 

Mipango ya huko nyuma ya Marekani kuhusu kadhia ya Palestina pia ilishindwa na kugonga ukuta kwa sababu kimsingi haikutambua haki ya Wapalestina ya kuwa na nchi huru, mji mkuu wake ukiwa Quds. Serikali ya Donald Trump pia imekariri makosa hayo hayo katika mpango wa Muamala wa Karne ambao hautambui haki yoyote ya Wapalestina katika mji wa Quds, na ukweli huu unaonekana vyema zaidi katika hatua ya Marekani ya kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv na kuupeleka Quds kinyume kabisa na maazimio ya kimataifa. Sera na siasa za Marekani daima ni kuuunga mkono na kuukingia kifua utawala ghasibu wa Israel na kwa sababu hiyo Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas, ametangaza kuwa, anapinga upatanishi wa Marekani katika kadhia ya Palestina.

Alaa kulli hal, baada ya kujulikana baadhi ya vipengee vya mpango wa eti "Muamala wa Karne" na uungaji mkono kamili wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni, Wapalestina wameamua kutangaza upinzani wao dhidi ya upatanishi wa Donald Trump ambaye hatambui rasmi moja kati ya matukufu yao yaani Baitul Muqaddas. 

 Ismail Hania

Kama alivyosema Mkuu wa Idara ya Siasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) Ismail Hania, msingi wa stratijia ya Wapalestina ni Quds, haki ya kurejea wakimbizi katika nchi yao na kuundwa nchi huru katika ardhi yote ya Palestina mji mkuu wake ukiwa Quds.