Makundi ya mapambano ya Palestina yataka kushadidishwa Intifadha ya Quds
(last modified Thu, 21 Apr 2016 03:49:34 GMT )
Apr 21, 2016 03:49 UTC
  • Makundi ya mapambano ya Palestina yataka kushadidishwa Intifadha ya Quds

Makundi ya mapambano ya Palestina yametoa wito wa kushadidishwa Intifadha ya Quds dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Makundi hayo ya mapambano ikiwemo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas na Jihad al-Islami yametoa taarifa inayosisitiza juu ya udharura wa kudumisha mapambano na kushadidishwa Intifadha katika maeneo mbalimbali ya ardhi za Palestina. Taarifa ya makundi hayo imebainisha kuwa, kunendelezwa mapambano ndiko kutakakoulazimisha utawala wa Kizayunin kurejee nyuma na kuondoka katika maeneo unayoyakalia kwa mabavu.

Tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka uliopita hadi sasa maeneo mbalimbali ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu yamekuwa yakishuhudia wimbi la malalamiko ya upinzani dhidi ya siasa za kichokozi za utawala wa Kizayuni na njama za utawala huo za kuvuruga utambulisho wa Baitul Muqaddas pamoja na mpango wake wa kuugawa kiwakati na kimahali msikiti mtukufu wa Al-Aqsa.

Wimbi hilo la malalamiko limekuwa maarufu kwa jina la Intifadha ya Quds.

Wapalestina zaidi ya 210 wameshauawa shahidi tangu ilipoanza Intifadha ya Quds mwezi Oktoba mwaka jana hadi hivi sasa.