Aug 08, 2019 08:03 UTC
  • OIC yatahadharisha kuhusu kuendelea jinai za Israel huko Palestina

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imetahadharisha kuhusiana na kuendelea hujuma na uvamizi wa wanajeshi wa Israel pamoja na walowezi wa Kizayuni huko Quds inayokaliwa kwa mabavu hususan wito uliotolewa na Wazayuni wa kuvamiwa Msikiti wa al-Aqswa.

Ahmad Rwaidy, balozi na mwakilishi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) huko Palestina ametahadharisha kwamba, hujuma, uvamizi na jinai za utawala ghasibu wa Israel huko Quds zinalivuta eneo hilo takatifu upande wa vita.

Balozi na mwakilishi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) huko Palestina amesisitiza juu ya umuhimu wa kuweko himaya na uungaji mkono wa Jumuiya ya Waqfu wa Kiislamu na Kikristo kwa mji wa Baytul-Muqaddas pamoja na wakazi wake mkabala na uadui na njama za kila uchao za utawala wa Israel.

Walowezi wa Kiizayuni wakivamia msikiti wa al-Aqswa

Kadhalika balozi Ahmad Rwaidy amesema kuwa, walowezi wa Kizayuni pamoja na wanajeshi wa Israel wamekuwa wakiendeleza jinai zao dhidi ya taifa la Palaestina. 

Hivi majuzi pia, Sheikh Mohamed Ahmed Hossein Mufti Mkuu wa mji wa Quds huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu alitahadharisha kuhusiana na hujuma na uvamizi wa Wazayuni dhidi ya msikiti mtakatifu wa al-Aqswa, kibla cha kwanza cha Waislamu.

Mufti Mkuu wa Quds alionya kuwa, Wazayuni wanafanya njama za kubadilisha utambulisho wa msikiti huo mtakatifu na kuwatwisha walimwengu kitu kingine ambacho kinakwenda kinyume na uhalisia wa mambo huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Tags