Saudi Arabia na Bahrain, "makuwadi wa kisiasa" wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i55274-saudi_arabia_na_bahrain_makuwadi_wa_kisiasa_wa_marekani
Marekani imekuwa ikiitisha vikao na mikutano kwa shabaha ya kutangaza sera zake za kueneza propaganda chafu dhidi ya Iran na sasa vikao hivyo vinafanyika katika nchi ndogo ya Bahrain.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 09, 2019 03:43 UTC
  • Saudi Arabia na Bahrain,

Marekani imekuwa ikiitisha vikao na mikutano kwa shabaha ya kutangaza sera zake za kueneza propaganda chafu dhidi ya Iran na sasa vikao hivyo vinafanyika katika nchi ndogo ya Bahrain.

Serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani inatumia kila kinachowezekana kupeleka mbele sera za siasa zake hizo katika kanda ya magharibi mwa Asia na Ghuba ya Uajemi. Siasa hizo zimelenga moja kwa moja usalama wa maeneo hayo, na kuletwa vikosi vya majeshi ya kigeni katika kanda hiyo kuna uhusiano mkubwa na sera na siasa hizo za serikali ya Washington. 

Kwa kutumia sera za kuzitisha nchi mbalimbali za magharibi mwa Asia na Ghuba ya Uajemi kuhusiana na kile kinachodaiwa ni "hatari ya Iran", Marekani imekuwa ikidhamini maslahi yake ya kiuchumi kupitia njia ya kuziuzia silaha na zana za kivita nchi za Kiarabu za eneo hilo. Hata hivyo ili kuweza kutimiza malengo yake, Washington inahitajia ushirikiano wa baadhi ya nchi za Ghuba ya Uajemi ikiwemo Saudi Arabia na Bahrain. Katika uwanja huu Saudi Arabia inatoa mchango wa kiuchumi na Bahrain inachukua nafasi ya kuwadi wa kisiasa wa Marekani. 

Mfalme wa Bahrain akitoa mkono wa utiifu....

Katika fremu hiyo hiyo Jumatano iliyopita Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo alifanya mazungumzo ya simu na mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, Muhammad bin Salman na pande hizo mbili zilijadili usalama wa safari za baharini na nafasi ya Iran katika eneo la Ghuba ya Uajemi. Pempeo alidai katika mazungumzo hayo kwamba, Saudi Arabia ni nchi yenye taathira kubwa katika kulinda usalama wa baharini katika eneo hilo. Sera hizo za Marekani zina uhusiano na mipango ya serikali ya Washington ya kukamua "gombe la maziwa" na kupata mabilioni ya dola za mafuta za Saudia. Vilevile kuchaguliwa Bahrain kwa ajili ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa kujadili usalama wa safari za baharini hapo tarehe 21 na 22 mwezi Oktoba mwaka huu ni utangulizi wa mchezo mpya wa Marekani katika eneo la Asia magharibi na Ghuba ya Uajemi. 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Sayyid Abbas Mousavi Alkhamisi ya jana aliashiria suala la kuchaguliwa Bahrain kuwa mwenyeji wa mkutano huo na kusema: "Mikutano kama hiyo inafanyika kwa ajili ya kuvuruga amani na usalama wa kanda ya magharibi mwa Asia na kutayarisha uwanja wa kutumwa vikosi vya majeshi ya nchi za kigeni na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kanda ya Ghuba ya Uajemi."

Sayyid Abbas Mousavi

Saudi Arabia na Bahrain ni mbawa mbili za utekelezaji wa siasa za Marekani katika kanda ya Ghuba ya Uajemi, na hapana shaka kuwa misimamo iliyodhidi ya Iran ya nchi hizo mbili za Kiarabu inapata maana na kuonekana vyema zaidi katika fremu hiyo. Hii ni licha ya kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara na kuziambia nchi za Kiarabu za kandokando ya Ghuba ya Uajemi kwamba, usalama wa eneo hilo utalindwa kwa ushirikiano wa nchi zote za kanda hiyo na kwamba, kuwepo majeshi ya kigeni katika kanda hiyo kunazidisha hali ya ukosefu wa amani na hitilafu kati ya nchi jirani.

Vilevile msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, usalama wa nchi za kanda hiyo hauwezi kutenganishika na hakuna nchi inayoweza kupata usalama na amani kwa kuvuruga usalama na amani ya nchi nyingine; hivyo inatarajiwa kuwa, nchi zote za kanda hii zitachukua hatua za kuzuia uingiliaji kati wa nchi za kigeni unaochochea hitilafu na migawanyiko. 

Mrithi wa kiti cha ufalme Saudia, Bin Salman akifundwa..

Inatupasa kusema hapa kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa nchi yenye taathira kubwa katika eneo la magharibi mwa Asia, ina nafasi muhimu sana katika kulinda usalama na amani ya safari za baharini katika kanda ya Ghuba ya Uajemi na lango bahari la Hormuz. Hivyo, kwa kutumia "tawala kuwadi" kama Bahrain, Marekani haiwezi kupuuza wala kufumbia macho mchango na nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuleta majeshi haramu katika eneo la Ghuba ya Uajemi.