Tahadhari ya Batalioni za Hizbullah ya Iraq kwa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i55557-tahadhari_ya_batalioni_za_hizbullah_ya_iraq_kwa_marekani
Batalioni za Hizbullah ya Iraq zimetoa taarifa zikiitahadharisha Marekani kuhusiana na kuendeleza mashambulizi dhidi ya kambi na vituo vya harakati ya wananchi ya nchi hiyo ya al Hashdu al Shaabi.
(last modified 2026-02-26T05:06:13+00:00 )
Aug 24, 2019 02:40 UTC
  • Tahadhari ya Batalioni za Hizbullah ya Iraq kwa Marekani

Batalioni za Hizbullah ya Iraq zimetoa taarifa zikiitahadharisha Marekani kuhusiana na kuendeleza mashambulizi dhidi ya kambi na vituo vya harakati ya wananchi ya nchi hiyo ya al Hashdu al Shaabi.

Vituo vya kijeshi vya al Hashdu al Shaabi nchini Iraq Jumanne iliyopita vilishambuliwa kwa mara ya nne katika mwezi mmoja uliopita na kuteketezwa. Vituo hivyo vilivyoshambuliwa ni Amerli , Abu Muntadhar al-Muhammadawi, al Saqr na al Balad. 

Kaimu Mkuu wa al Hashdu al Shaabi, Abu Mahdi al-Mohandes amesema katika taarifa yake kwamba, Wamarekani wameingiza Iraq ndege nne zisizo na rubani kutoka Israel kwa ajili ya kushambulia vituo na kambi za Iraq na kuongeza kuwa: "Marekani ndiyo inayohusika na yote yanayotokea Iraq na inabeba dhima ya matukio hayo yote." 

Wanamapambano wa Hizbullah ya Iraq

Swali linalojitokeza hapa ni kwamba, Marekani na Israel zinafuatilia malengo gani katika mashambulizi yao dhidi ya vituo na kambi za al Hashdu al Shaabi?

Jibu la kwanza ni kwamba, harakati ya al Hashdu al Shaabi ni mchezaji mpya lakini mwenye satua na ushawishi mkubwa katika uwanja wa siasa na usalama wa Iraq na ilitoa mchango mkubwa sana katika kulishinda na kuliangamiza kundi la kigaidi la Daesh nchini humo. Japokuwa Marekani ilianzisha kile kilichopewa jina la Muungano wa Kimataifa wa Kupambana na Daesh nchini Iraq lakini uchunguzi makini umebaini kuwa, Marekani haitaki kuangamizwa kabisa kundi hilo la kigaidi nchini Iraq bali inataka kubakishwa "Daesh dhaifu" ambayo inalinda na kuoana na maslahi yake. Hivyo harakati ya al Hashdu al Shaabi iliyoanzishwa kwa fatuwa ya kiongozi mkuu wa kidini wa Iraq na jeshi la nchi hiyo vimezima njama na mipango hiyo na Marekani. 

Vilevile katika uchaguzi wa Bunge wa mwaka jana nchini Iraq harakati ya al Hashdu al Shaabi ilishika nafasi ya pili kwa kushinda idadi kubwa ya viti vya Bunge baada ya kundi la Sairoon linaloongozwa na Muqtada al Sadr. Tukio hilo lilionesha kuwa, harakati hiyo pia ni mchezaji mahiri na hodari katika medani ya siasa. Vilevile kutokana na kwamba, kidhati, al Hashdu al Shaabi inahesabiwa kuwa katika kambi ya harakati za Muqawama zinazopinga uingiliaji kati wa Marekani katika masuala ya Asia magharibi na inautambua utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni adui, kunashuhudiwa mgongano wa kiutambulisho na kidhati baina yake na Marekani na Israel. Kwa msingi huo, Marekani na Israel zimeamua kushambulia vituo na kambi za harakati ya al Hashdu al Shaabi ili kuzuia mafanikio ya harakati hiyo katika muundo wa kisiasa na madaraka wa Iraq na kupunguza nguvu ya kambi ya Muqawama katika eneo la Asia magharibi. 

Wapiganaji wa al Hashu al Shaabi, Iraq

Lengo jingine la mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya vituo na kambi za al Hashdu al Shaabi ni kutaka kueneza propaganda chafu kwamba, kuna hitilafu na mgawanyiko mkubwa baina ya al Hashdu al Shaabi na Waislamu wa madhehebu ya Ahlusunna  nchini Iraq. Hii ni kwa sababu, baadhi ya kambi za harakati hiyo zipo katika maeneo ya Wasuni. 

Lengo la tatu la mashambulizi hayo ni kutaka kuathiri na kuvuruga mafanikio ya kambi ya Muqawama nchini Syria. Jeshi la Syria na waitifaki wake limeanza hatua ya mwisho ya kuyaangamzia kabisa makundi ya kigaidi katika operesheni inayoendelea katika mko wa Idlib, na mashambulizi dhidi ya kambi na vituo vya al Hashdu al Shaabi yamefanyika sambamba na operesheni ya Idlib. 

Firas al Yasiri ambaye ni mjumbe wa Baraza la Siasa la harakati ya al Nujabaa ya Iraq anasema: "Marekani inataka kuyadhibiti maeneo ya magharibi hususan maeneo ya wazi yanayopakana na Syria au Jordan na kuyatumia kwa ajili ya kuhudumia malengo yake na vilevile kuyalenga makundi ya Muqawama." 

Lengo au sababu ya nne ni kwamba, Marekani na Israel zinatumia mashambulizi dhidi ya kambi na vituo vya al Hashu al Shaabi kutaka kuvuruga uhusiano wa Iraq na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Uhusiano wa nchi hizo mbili ndugu na jirani ni wa kirafiki na unaendelea kuimarika siku baada ya siku. Kupitia mashambulizi dhidi ya kambi na vituo vya al Hashdu al Shaabi, Marekani na Israel zinataka kutoa ujumbe kwamba, japokuwa haziwezi kuishambulia Iran na Hizbullah huko Lebanon lakini zinaweza kumlenga muitifaki wao mpya na kuzuia mafanikio yao ndani ya Iraq na katika kanda ya magharibi mwa Asia.

Wamarekani hawataku kuona kundi la kigaidi la Daesh likiangamizwa kikamilifu

Pamoja na hayo yote Marekani na Israel zinapaswa kutilia maanani tahadhari iliyotolewa na Batalioni za Hizbullah ya Iraq. Tahadhari hiyo inawaambia wanajeshi wa Marekani kwamba: "Kambi zenu haziwezi kulinda usalama wenu na zinaweza kulengwa kwa makombora yetu. Kama kutaanza mpambano basi jueni kwamba, hautamalizika isipokuwa kwa kuwafukuzeni kikamilifu katika eneo lote la Mashariki ya Kati."