UNICEF: Watoto milioni 2 wamekatiziwa masomo Yemen kutokana na vita
(last modified Thu, 26 Sep 2019 04:13:28 GMT )
Sep 26, 2019 04:13 UTC
  • UNICEF: Watoto milioni 2 wamekatiziwa masomo Yemen kutokana na vita

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umesema watoto zaidi ya milioni mbili nchini Yemen wameshindwa kuendelea na masomo yao kutokana na vita vinavyoshuhudiwa nchini humo.

Katika taarifa jana Jumatano, Sara Beysolow Nyanti, mjumbe wa UNICEF nchini Yemen alisema akthari ya watoto hao walikatiziwa masomo yao baada ya kuanza mashambulizi ya muungano wa kijeshi wa Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo maskini mnamo Machi 2015.

Amesema moja katika kila shule tano nchini Yemen zimeharibiwa kikamilifu kutokana na athari za moja kwa moja za vita hivyo, hususan mashambulizi ya anga.

Afisa huyo wa UNICEF ameeleza bayana kuwa, "Mustakabali wa elimu ya watoto milioni 3.7 wa Yemen haufahamiki, kwa kuwa walimu wengi wameacha kazi ya kufundisha kwa kutolipwa mishahara kwa zaidi ya miaka miwili sasa." 

Watoto ndio wahanga wakuu wa mashambulizi ya Saudia nchini Yemen

Kwa mujibu wa takwimu za shirika hilo la watoto la Umoja wa Mataifa, watoto wapatao 7,300 wameuawa nchini Yemen katika vita na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia na washirika wake tokea mwaka 2015 hadi sasa.

UNICEF imesema katika kila saa 24 nchini Yemen, mtoto mmoja ima huuawa, kujeruhiwa au kuingizwa vitani kwa nguvu, na kwamba katika kila dakika 10, mtoto mmoja nchini Yemen hufariki dunia kutokana na magonjwa au sababu zinazoweza kuzuilika.