Hizbullah: Hatutosalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i56535-hizbullah_hatutosalimu_amri_mbele_ya_mashinikizo_ya_marekani
Naibu Mkuu wa Baraza la Utendaji la Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa vikwazo vya Marekani haviwezi kudhoofisha imani na ahadi yake ya kulinda nchi na raia.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Oct 10, 2019 08:37 UTC
  • Hizbullah: Hatutosalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani

Naibu Mkuu wa Baraza la Utendaji la Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa vikwazo vya Marekani haviwezi kudhoofisha imani na ahadi yake ya kulinda nchi na raia.

Sheikh Ali Damush ameashiria pia juu ya njama endelevu za Marekani na utawala haramu wa Kizayuni Israel zenye njozi ya kuusambaratisha muqawama katika eneo la Asia Magharibi na kuongeza kuwa, Hizbullah haitosalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani. Sheikh Ali Damush amefafanua kuwa, vikwazo vya Marekani dhidi ya Lebanon ni vita vya kiuchumi dhidi ya raia wa nchi hiyo na kuongeza kwamba, mashinikizo ya leo ya Washington ni yenye lengo la kutaka kuvunja umoja wa taifa la Lebanon, lakini kamwe Hizbullah haitoruhusu maslahi ya wananchi yaingie hatarini na kuipeleka nchi kwenye mkondo wa kusambaratika. 

Sheikh Ali Damush, Naibu Mkuu wa Baraza la Utendaji la Harakati ya Hizbullah ya Lebanon 

Inafaa kuashiria kuwa, baada ya harakati hiyo ya muqawama kupata mafanikio makubwa katika mapambano yake dhidi ya makundi ya kigaidi na ukufurishaji katika eneo, Marekani na utawala haramu wa Israel zimezidisha mashinikizo dhidi ya harakati hiyo ambapo Washington imezifunga akaunti za benki za shakhsia kadhaa wa Lebanon kwa tuhuma za kuwa na uhusiano na harakati ya Hizbullah.