Nov 09, 2019 07:52 UTC
  • Idadi ya askari wanaokimbia kuhudumu jeshini Israel yaongezeka

Idadi ya askari wanaokimbia kuhudumu ndani ya jeshi la utawala haramu wa Kizayuni Israel, imezidi kuongezeka huku suala la matatizo ya kisaikolojia likitajwa kuwa ndio sababu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, askari wanaokimbia kuhudumu ndani ya jeshi hilo wameongezeka maradufu ambapo wamekuwa wakipata msamaha kwa kutumia kisingizio cha matatizo ya kisaikolojia. Gazeti la Kizayuni la Maariv limefichua kwamba kwa mujibu wa ripoti za jeshi la Israel mwaka jana, kiwango cha askari waliopata msamaha wa kuhudumu jeshini, kiliongezeka kwa asilimia 30. Uchunguzi uliofanywa kuhusiana na takwimu zinazohusiana na suala hilo, unaelezea kuwepo hali isiyo ya kawaida nayo ni ongezeko la asilimia 100 la watu wanaowasilisha nyaraka zinazoonyesha mateso yanayosababishwa na matatizo ya kisaikolojia ili wapate msamaha. Kabla ya hapo mtandao wa habari wa al-Ahd wa nchini Lebanon uliandika kwamba, hali ya kukata tamaa askari wa Israel, imepelekea ongezeko kubwa la askari wanaojiua ndani ya jeshi hilo la Kizayuni.

Askari wa utawala haramu wa Israel 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, jeshi la Israel kutakiwa kuwa katika hali ya tahadhari ya hali ya juu wakati wote, kumewafanya askari wa utawala huo katili kukata tamaa na kukosa hamu ya kuendelea kuhudumu jeshini, hasa kwa kuwa askari hao wanakosa muda wa mapumziko. Kadhalika ripoti hiyo imeongeza kwamba, ongezeko la nguvu za wanamuqawama wa Ukanda wa Gaza, Lebanon na Syria katika uga wa makombora, silaha na ujasiri wao wa kimapambano, ni mambo yaliyodhoofisha moyo wa askari hao wa utawala haramu wa Israel.

Tags