Mashambulizi ya anga ya Israel yaua shahidi makumi ya Wapalestina Gaza
Ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel jana Jumanne na kwa siku ya pili mfufulizo zilitekeleza mashambulizi ya anga zaidi ya 50 katika Ukanda wa Gaza, na kuua shahidi makumi ya Wapalestina.
Ashraf al-Qidra, msemaji wa Wizara ya Afya katika Ukanda wa Gaza amesema Wapalestina wasiopungua 24 wameuawa kufuatia mashambulizi hayo ya anga ya jeshi katili la Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza, huku wengine wengi wakijeruhiwa.
Aidha vifaru vya utawala huo haramu vimetekeleza mashambulizi 21 dhidi ya Wapalestina katika eneo la Khan Younis na kuua shahidi wawili miongoni mwao.
Baadhi ya vyombo vya habari vya Palestina vimeripoti kuwa, watu zaidi ya 70 wamejeruhiwa katika hujuma hizo za anga na za nchi kavu za utawala pandikizi wa Israel dhidi ya Gaza, mbali na kuharibu majumba, mashamba ya kilimo na miundombinu.
Mapema Jumatatu, jeshi la Israel lilifanya mashambulizi ya kinyama dhidi ya eneo la Gaza na baadhi ya viunga vya mji wa Damascus, Syria ambapo maafisa wa ngazi za juu wa harakati ya muqawama ya Jihadul-Islami waliuawa.
Nchi na taasisi za kimataifa ikiwemo Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC zimetoa taaria za kulaani mashambulizi hayo ya kinyama ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Gaza.