Nov 15, 2019 07:58 UTC
  • Jumuiya ya Al-Wifaq: Bahrain imegeuzwa na kuwa jela kubwa

Jumuiya ya Mwafaka wa Kiislamu na Kitaifa nchini Bahrain (Al Wifaq) imetangaza kuwa, hatua za utawala wa nchi hiyo wa Aal Khalifa zimeigeuza Bahrain na kuwa jela kubwa.

Taarifa ya Jumuiya ya Mwafaka wa Kiislamu na Kitaifa nchini Bahrain (Al Wifaq) imeeleza kuwa, hatua ya utawala wa kifamilia wa Aal-Khalifa za kufanya ukandamizaji na mbinu nyingine zisizo za kisheria zimeifanya nchi hiyo kugeuka na kuwa jela kubwa ambayo ndani yake hakuna mtu mwenye haki ya kusema hata neno moja.

Taarifa ya jumuiya hiyo imekosoa vikali pia kimya cha jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa dhidi ya ukandamizaji unaofanywa nchini Bahrain dhidi ya raia wanaotaka mageuzi na uhuru wa kisiasa.

Maandamano ya wananchi wa Bahrain

Sehemu moja ya taarifa hiyo imeonyesha kusikitishwa na hatua za jamii ya kimataifa na asasi za kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa za kuamua kutia pamba masikioni na kupuuza kilio cha wananchi wa Bahrain.

Nchi ya Bahrain ni kisiwa kidogo kilichoko katika Ghuba ya Uajemi ambapo utawala wa kifamilia wa Aal Khalifa ndiyo unaotawala nchini humo. Dhulma, ukandamizaji, utumiaji mabavu na ubaguzi ni sifa kuu za watawala wa ukoo wa Aal Khalifa katika nchi hiyo ndogo ya Kiarabu.

Katika kipindi cha miaka saba iliyopita, utawala wa Aal Khalifa umewatia nguvuni zaidi ya raia 11,000 wa Bahrain kwa tuhuma bandia, ambapo baadhi yao wamenyongwa na wengine wengi wamenyang'anywa uraia au kufukuzwa nchini humo.

Tags