Harakati ya Hashdush-Sha'abi yategua mabomu 100 nchini Iraq
Harakati ya Wananchi ya Hashdush-Sha'abi nchini Iraq imefanikiwa kutegua mabomu 100 pamoja na mada za miripuko katika mkoa wa Kirkuk, kaskazini mwa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na harakati hiyo imesema kuwa, Jumatano ya jana kikosi cha 16 cha Hashdush-Sha'abi kilitegua mabomu 100 pamoja na mada za miripuko katika mkoa huo. Kwa mujibu wa habari hiyo mabomu hayo yalikuwa yametegwa katika eneo la Tal Ahmad katika mkoa huo ambapo yaligunduliwa kupitia operesheni zilizofanywa na wanachama wa harakati hiyo. Hii ni katika hali ambayo Jumapili iliyopita pia wanamuqawama wa harakati ya wananchi nchini Iraq walifanya operesheni katika makao makuu ya magaidi wa Daesh katika mkoa wa Diyala, mashariki mwa nchi na kufanikiwa kuisambaratisha ngome hiyo.
Kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh lilikuwa likiitumia ngome hiyo kwa ajili ya kutoa mafunzo ya kigaidi katika mkoa wa Diyala, Kirkuk na Saladin. Hatua ya saba ya operesheni ya irada ya ushindi kwa kushirikiana na askari wa serikali ya Iraq, ilianza siku ya Jumamosi iliyopita katika maeneo manne ya mikoa ya Diyala na Saladin, mashariki na kaskazini magharibi mwa Iraq. Baada ya kulishinda kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) nchini humo, wapiganaji wa kujitolea kwa kushirikiana na jeshi la taifa hilo wangali wanaendeleza operesheni za kusaka mabaki ya magaidi wa genge hilo katika maeneo tofauti ya Iraq.