Waziri Mkuu mpya wa Lebanon; vipaumbele vyake na changamoto zinazomkabili
Rais Michel Aoun wa Lebanon amemtangaza Hassan Diab, shakhsia miongoni mwa Waislamu wa madhehebu ya Sunni na waziri wa zamani wa elimu ya juu wa nchi hiyo, kuwa waziri mkuu mpya na kumpa jukumu la kuunda serikali.
Tangu tarehe 17 Oktoba, Lebanon imekuwa ikishuhudia maandamano ya upinzani, ya wananchi wanaolalamikia hali mbaya ya uchumi na ufisadi uliokithiri nchini humo. Tarehe 29 Oktoba, zikiwa zimepita siku 13 tu tangu yalipoanza maandamano hayo, Waziri Mkuu Saad Hariri alijiuzulu wadhifa wake huo. Katika muda wote wa siku 50 zilizofuatia baada ya hapo, yametajwa majina tofauti ya watu waliofikiriwa kwamba wataweza kukalia kiti cha uwaziri mkuu wa Lebanon, huku Hariri akionekana kuwa na nafasi kubwa zaidi kulinganisha na majina mengine yaliyopendekezwa.
Hata hivyo kuhitalifiana Saad Hariri na makundi mengine ya kisiasa ya Lebanon, sisitizo lake la kuunda serikali ya mateknokrati watupu na kupinga serikali ya mchanganyiko wa wanasiasa na mateknokrati na vilevile utegemezi wa kupindukia alionao yeye mwenyewe kwa maajinabi, yote hayo, yalimfanya hatimaye aghairi kuunda serikali nyingine mpya.
Mtu anayependekezwa kushika wadhifa wa uwaziri mkuu wa Lebanon inapasa awe amepata asilimia 50 jumlisha na moja ya kura za bunge, ambazo ni kura zisizopungua 65 miongoni mwa kura 128 za wabunge wote. Katika kikao cha bunge kilichofanyika jana, Hasasan Diab alipata kura 69 kati ya kura za wabunge wote na hivyo kumwezesha kuwa na mamlaka ya kuunda baraza jipya la mawaziri. Kutangazwa Diab kuwa waziri mkuu mpya wa Lebanon kunamaanisha kupata ushindi muungano wa Muqawama katika mchuano huo wa kisiasa kupitia bunge, kwa sababu mgombea huyo ameungwa mkono na mrengo wa muqawama katika bunge la nchi hiyo.
Si hayo tu, bali kuchaguliwa Hsssan Diab kuwa waziri mkuu wa Lebanon maana yake ni kuachia rasmi Saad Hariri hatamu za madaraka ya nchi, ingawa ni kwa kulazimika na bila ya kupenda. Kukabidhiwa Diab jukumu la kuunda serikali mpya ya Lebanon vile vile kunaonyesha kuwa, mbinu ya "kujiuzulu ili kufanya muamala wa kisiasa na kujipatia fursa zaidi" ambayo ameitumia Hariri, imetokana na mahesabu tasa aliyofanya kuhusu nafasi ya mirengo mingine ya kisiasa ya nchi hiyo; na tab'an imesababishwa pia na udhaifu wake wa kutegemea madola ya kigeni na hasa Saudi Arabia, ambao hatimaye umemfanye atupwe nje ya ulingo wa madaraka.
Kushughulikia matakwa ya kiuchumi na kijamii ya wananchi, kitakuwa kipaumbele muhimu zaidi kwa waziri mkuu mpya wa Lebanon. Baada ya kukabidhiwa rasmi jukumu la kuunda serikal, Diab alisema: "Uwazi na kupambana na ufisadi" vitakuwa katika ajenda zitakazofanyiwa kazi.
Lakini pamoja na hayo, kuna changamoto muhimu pia ambazo waziri mkuu mpya wa Lebanon atakabiliana nazo.
Changamoto ya kwanza inahusu mwenendo wa Harakati ya Machi 14, na hasa Harakati ya Al-Mustaqbal inayoongozwa na Saad Hariri. Katika kikao cha jana cha bunge la Lebanon, wabunge 44, wakiwemo 18 wa Harakati ya Al-Mustaqbal na 14 wanaowakilisha harakati ya Kikristo ya Quwaatul-Lubnaniyah inayoongozwa na Samir Jaajaa, hawakushiriki katika upigaji kura. Mwenendo huo usio wa uwajibikaji katika kuamiliana na uchaguzi wa waziri mkuu mpya unamaanisha kwamba, katika mchakato wa uundaji serikali mpya pia, harakati hizo, sio tu hazitatoa ushirikiano, lakini inawezekana hata zikafanya uafriti wa kukwamisha mchakato huo.
Changamoto ya pili muhimu inayomkabili Diab ni uingiliaji na mashinikizo tarajiwa kutoka nje. Kwa kuzingatia kwamba Hassan Diab amefanikiwa kushika hatamu za uwaziri mkuu kwa uungaji mkono wa muungano wa muqawama bungeni, kambi ya pande nne ovu inayoundwa na Marekani, Israel, Saudi Arabia na Imarati itafanya kila aina ya uafriti dhidi ya Diab katika mchakato wa uundaji serikali na pia baada ya kuunda serikali mpya ya Lebanon.
Changamoto ya tatu muhimu iliyopo ni kwamba Diab anarithi uozo na matatizo chungu nzima ya kiuchumi na wimbi kubwa la mangung'uniko na malalamiko ya wananchi, ambayo ni mabaki ya Saad Hariri na serikali yake iliyojiuzulu.
Lakini kwa kumalizia inapasa tuseme kwamba, kukivuka kigingi cha fujo na machafuko ya miezi miwili yaliyoshuhudiwa nchini Lebanon na kuweza kuwatuliza wananchi au angalau kupoza moto wao wa manung'uniko kunahitaji "muda" na "uungaji mkono" wa mihimili mingine ya madaraka ya nchi hiyo.../