Arab League yailaani Brazil kwa kufungua ofisi ya kibiashara Quds tukufu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i58004-arab_league_yailaani_brazil_kwa_kufungua_ofisi_ya_kibiashara_quds_tukufu
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imeikosoa vikali Brazil kwa kufungua ofisi ya kibiashara katika mji wa Quds huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.
(last modified 2025-10-22T08:58:50+00:00 )
Dec 20, 2019 11:42 UTC
  • Arab League yailaani Brazil kwa kufungua ofisi ya kibiashara Quds tukufu

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imeikosoa vikali Brazil kwa kufungua ofisi ya kibiashara katika mji wa Quds huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.

Arab League ilipasisha azimio la kulaani hatua hiyo ya kichokozi ya Brazil katika kikao cha dharura kilichofanyika jana Alkhamisi katika mji mkuu wa Misri, Cairo ambapo imesisitiza kuwa, kitendo hicho kinaonyesha ni jinsi gani Brazil inaendelea kukiuka sheria za kimataifa.

Taarifa ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imesema, " Hatua hiyo ya upande mmoja na iliyo kinyume cha sheria inaashiria uungaji mkono wa Brazil kwa vitendo haramu na sera batili za Israel zenye lengo la kulidhibiti eneo la mashariki mwa Quds (Jerusalem)."

Bendera za Brazil na utawala haramu wa Israel

Wakati huohuo, Kuwait na Algeria zimetoa taarifa ya kulaani hatua hiyo ya Brazil ya kufungua Ofisi ya Biashara huko Quds tukufu, zikisisitiza kuwa kitendo hicho hakitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kushadidisha taharuki katika eneo la Asia Magharibi, sanjari na kudhalilisha mchakato wa kupatiwa ufumbuzi mgogoro wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Palestina. 

Brazil ni katika nchi chache duniani zinazoutambua mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel kuwa eti ni mji mkuu wa utawala huo pandikizi, ingawa hadi sasa haijauhamishia ubalozi wake katika mji huo.

Tayari Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu OIC imeitahadharisha Brazil dhidi ya mpango wake wa kuuhamishia ubalozi wake katika mji wa Quds kutoka Tel Aviv, ikisisitiza kwamba hatua hiyo itakuwa na athari mbaya katika uhusiano wa nchi hiyo ya Amerika ya Latini na nchi za Kiislamu na za Kiarabu.