Kiwewe cha Pompeo kuhusu matukio ya hivi karibuni mjini Baghdad, Iraq
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo sambamba na kukariri madai yake bandia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema kwamba matukio ya mjini Baghdad, yanatishia maslahi ya nchi yake.
Pompeo ameyasema hayo asubuhi ya leo Januari Mosi 2020 katika mahojiano na kanali ya CBS ambapo akikariri madai yake ya siku zote amedai kwamba eti Iran inaunga mkono ugaidi. Aidha amesema kuwa ubalozi wa Marekani mjini Baghdad uko salama na kwamba Washington imechukua hatua zote kwa ajili ya kulinda usalama wa raia wake. Ameelezea jukumu la viongozi wa Iraq la kudhamini usalama wa taasisi za Marekani na kudai kwamba shambulizi lililofanywa na watu aliowataja kuwa ni magaidi dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Baghdad, lilikuwa limeratibiwa.
Hii ni katika hali ambayo ripoti zinaarifu kwamba Washington imewahamisha wafanyakazi wa ubalozi wake 80 mjini Baghdad na kuwapeleka mji wa Erbil katika eneo la Kurdistan. Hatua hiyo ilichukuliwa kufuatia shambulio tarajiwa dhidi ya ubalozi huo, baada ya jeshi la Marekani kushambulia ngome za Harakati ya Hashdu sh-Sha'abi katika eneo la Al-Qaim la mkoa wa Al-Anbar na kuwaua shahidi makumi ya wanamuqawama wa harakati hiyo. Hatua hiyo ya uvamizi ilikabiliwa na hasira kali ya raia wa Iraq kiasi kwamba baada ya mazishi ya mashahidi wa hujuma hiyo, maelfu ya Wairaqki walifanya maandamano makubwa mbele ya ubalozi wa Marekani mjini Baghdad wakipiga nara za 'Mauti kwa Marekani.'