Yemen yazitaka asasi za kimataifa kupamabana na maradhi ya kuambukiza
Maafisa wa sekta ya afya nchini Yemen wametoa wito kwa asasi za kimataifa kuongeza juhudi za kukabiliana na maradhi ya kuambukiza kama homa ya dengue na vilevile malaria.
Taarifa iliyotolewa na viongozi hao imetahadharisha kwamba, endapo maradhi ya malaria na homa ya dengue yataendelea kuenea nchini humo kuna uwezekano mkubwa wa kutokea vifo vingi.
Taasisi ya kimataifa ya Save The Children imetangaza katika taarifa yake kwamba, watoto 78 wameaga dunia kutokana na homa hatari ya dengue.
Asasi hiyo inayojishughulisha na masuala ya watoto imesisitiza kuwa, kuna watu wapatao 52,000 ambao wanashukiwa kuambukkizwa homa ya dengue katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Itakumbukwa kuwa Saudia kwa kushirikiana na Marekani, Israel, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi na Kiarabu ilianzisha mashambulizi makali ya kila upande dhidi ya Yemen hapo mwezi Machi 2015 sambamba na kuizingira nchi hiyo masikini ya Kiarabu kwa pande za nchi kavu, baharini na angani.
Vita vya Saudia na washirika wake nchini Yemen hadi sasa vimepelekea mauaji ya makumi ya maelfu ya watu huku malaki ya wengine wakijeruhiwa mbali na mamilioni ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi.
Hata hivyo Saudia na washirika wake wameshindwa kabisa kufikia malengo yao haramu ndani ya nchi hiyo kutokana na mapambano na kusimama kidete jeshi na wananchi wa nchi hiyo.