"ISIS walitaka kushambulia ubalozi wa Marekani Lebanon na kuisingizia Hizbullah"
Gazeti la al Jamhuriyyah la Lebanon limefichua kuwa, genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) lilikuwa limepanga njama za kushambulia ubalozi wa Marekani mjini Beirut ili kuibebesha lawama harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo Hizbullah hasa baada ya Marekani kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds, cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH.
Katika ripoti yake ya jana Alkhamisi, gazeti hilo lilifichua kuwa, maafisa usalama wa Lebanon wamezima shambulio hilo la kigaidi la Daesh kabla halijafanyika na kumtia mbaroni gaidi mmoja.
Gazeti hilo limeongeza kuwa, kama operesheni hiyo ya kigaidi ingelitokea, basi lawama zote zingelielekezwa kwa harakati ya Hizbullah ya Lebanon hasa kutokana na hali tete iliyopo katika eneo la Asia Magharibi hivi sasa baada ya wanajeshi magaidi wa Marekani kumuua kidhulma Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH huko nchini Iraq.
Kamanda Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliuliwa kidhulma na wanajeshi vamizi wa Marekani tarehe 3 mwezi huu wa Januari akiwa mgeni rasmi wa serikali ya Iraq. Luteni Soleimani aliuawa shahidi pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu wa Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq, al Hashd al Shaabi na wenzao wanane baada ya gari walilokuwa wamepanda kushambuliwa kutokea angani na wanajeshi magaidi wa Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad, nchini Iraq.
Hatua iliyofuatia baada ya ugaidi huo ni Bunge la Iraq kupasisha muswada wa kufukuzwa wanajeshi magaidi wa Marekani nchini humo. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nayo ilitoa majibu makali kwa kushambulia kwa makombora kambi mbili za wanajeshi vamizi wa Marekani nchini Iraq. Leo Ijumaa pia wananchi wa Iraq wameitisha maandamano ya milioni ya watu kushinikiza kufukuzwa wanajeshi vamizi wa Marekani nchini mwao.