Jeshi la Syria lakomboa kikamilifu kusini mwa mkoa wa Idlib
Taasisi inayoitwa 'Watetezi wa Haki za Binaadamu Syria' imetangaza kuwa jeshi la Syria limefanikiwa kukomboa kikamilifu kusini mwa mkoa wa Idlib, kaskazini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.
Jeshi la Syria Alhamisi ya jana lilifanikiwa kukomboa kikamilifu eneo la kusini mwa mkoa huo na kulidhibiti baada ya kusambaratisha ngome za magaidi katika eneo hilo. Kadhalika katika operesheni hizo, jeshi la Syria limefanikiwa kutwaa udhibiti wa ngome za magaidi katika maeneo ya Al Enkawi, Kulaidan, Al Huwaijah, Al Hawash, Hawash, Al-Amqiyah na Beit Raas, magharibi mwa jimbo la Hama, magharibi mwa nchi hiyo.
Operesheni za jeshi la Syria katika mikoa ya Idlib na Aleppo zilianza tarehe 24 Januari mwaka huu na hadi sasa bado zinaendelea. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, huku udhibiti wa jeshi la Syria kwa maeneo ya mikoa ya Aleppo, Idlib na Al-Hasakah ukiendelea, katika siku za hivi karibuni jeshi la Uturuki limeendelea kuyaunga mkono makundi ya kigaidi sambamba na kushambulia maeneo ya jeshi la Syria. Katika uwanja huo pia kumeripotiwa mapigano kati ya majeshi ya nchi mbili hizo katika maeneo hayo.