Kufeli siasa za Uturuki mkoani Idlib, Syria
Wajumbe wa kisiasa wa Russia na Uturuki wamekutana mjini Ankara kujadiliana masuala ya kaskazini mwa Syria hasa ya mkoa wa Idlib.
Kabla ya hapo pia wajumbe wa nchi hizo mbili walishakutana mara mbili, Ankara na Moscow, kujadiliana suala hilo hilo la mkoa wa Idlib, wa Syria.
Wataalamu wa mambo wanasema kuwa, uvamizi wa kijeshi wa Uturuki nchini Syria hasa huko Idlib umeiharibia jina nchi hiyo na kuwafanya watu wengi wasiyaamini tena madai ya Ankara ya kupambana na wafuasi wa chama cha Kikurdi cha PKK katika eneo hilo. Si hilo tu, lakini pia maadui wa Uturuki na hata Marekani, zinapenda kuiona Ankara inajichafulia jina na inajiingiza katika vita ambavyo vitavuruga uchumi wake.
Ukweli ni kwamba manufaa ya Uturuki na Russia kuhusiana na Syria ni tofauti bali yanakinzana.
Sasa hivi hali katika mkoa wa Idlib iko kwa namna ambayo imeilazimisha Uturuki kupata hasara kubwa ya kugharama uhai mfupi uliobakia wa magenge ya kigaidi. Karibuni tu hivi magenge hayo ya kigaidi yataangamizwa nchini Syria na wale watakaobakia hai kati ya magaidi hao imma watakimbia nchi au watajisalimisha kwa jeshi la Syria iwe sasa hivi au baadaye.
Uturuki nayo inalitambua vyema jambo hilo. Inaelewa kuwa magenge hayo ambayo yalishirikiana na magenge mengine ya kigaidi kama vile al Qaida na Daesh (ISIS) na kufanya jinai kubwa nno na zisizo na kifani katika maeneo waliyoyateka, kamwe hayawezi kupendwa na wananchi wa Syria na wala hayawezi kupewa nafasi ya kushiriki katika maamuzi ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Kwa miaka yote hii, magenge hayo mbali na kuwasababishia majanga makubwa wananchi wa Syria kwa kuangamiza kila kitu chao, yametumiwa pia kijasusi na madola ya kibeberu na muda wote yamekuwa ni mamluki tu wa maadui wa wananchi wa Syrian kiasi kwamba Uturuki imekuwa ikiwatumia magaidi hao hao kufanikishia malengo yake nchini Libya na mara kwa mara imekuwa ikiwasafirisha kutoka Syria hadi Libya kwenda kulinda maslahi yake katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Kuendelea mgogoro wa Syria na uingiliaji wa papara wa Uturuki katika mgogoro huo hauna matunda mengine isipokuwa kushadidisha hali tete iliyopo katika eneo hilo na Ankara haiwezi kusalimika na madhara ya mgogoro wa Syria kwani uko kwenye mipaka yake. Vile vile Uturuki ilipaswa kuelewa kuwa, siasa zake za kuendelea kuwakingia kifua magaidi huko Syria kunahatarisha maslahi yake ya muda mrefu nchini humo.
Uturuki inadhani kuwa itaweza kuishinikiza Russia kupitia kuyaunga mkono magenge ya kigaidi mkoani Idlib, Syria sambamba na kujiweka karibu na nchi za Magharibi. Lakini kabla ya jambo lolote, mtazamo huo unaonesha jinsi wasivyo makini watungaji wa sera za kigeni huko Uturuki. Ni hivi karibuni tu Uturuki iliuwekia katika hali nguvu uhusiano wake na nchi za Magharibi kutokana na kujikurubisha kwake kwa Russia. Ilifanya hivyo ili kuziweka nchi za Magharibi katika mashinikizo na kuzilazimisha ziifanyie Uturuki inachotaka. Hata hivyo inaonekana kwamba siasa na stratijia hizo za Uturuki zitafeli karibuni tu hivi kwa sababu, kadiri mchezo huo wa kisiasa utakavyoendelea ndivyo utakavyozidi kupoteza imani ya nchi nyingine kwa Uturuki. Siasa hizo zitaongeza idadi ya maadui wa Ankara ambao muda wote watakuwa wanasubiri kupata fursa ndogo tu ya kulipiza kisasi kutokana na "ulaghai" waliofanyiwa na Uturuki wa kujifanya leo iko pamoja nao na kesho inajigeuza na kuwa adui yao.