Harakati ya Jihad Islami ya Palestina yasisitiza kuendelea kuwatetea mateka Wapalestina
Harakati ya Jihad Islami ya Palestina imesisitiza kuwa itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuwatetea mateka Wapalestina wanaoshikiliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel ili hatimaye waachiliwe huru.
Katika taarifa, Harakati ya Jihad Islami imesema: "Sambamba na Siku ya Mateka Wapalestina (Aprili 17), utawala wa Kizayuni wa Israel ulianza kuwahujumu mateka Wapalestina inaowashikilia." Taarifa hiyo imesema utawala wa Kizayuni unatumia vibaya hali ya sasa ambapo dunia inashughulishwa na janga la corona kushadidisha hatua zake za kinyama dhidi ya mateka Wapalestina.
Jihad Islami imeutahadharisha utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusu jinai zake dhidi ya mateka Wapalestina na kusema utawala huo unabeba dhima kuhusu maisha na afya ya mateka hao.
Taarifa hiyo imesema Jihad Islami itatekeleza wadhifa wake kuhusu kulitetea taifa la Palestina na iko tayari kuingia katika mapambano ya kukomboa na kuwarejesha nyumbani wakimbizi na mateka Wapalestina.
Kwa mujibu wa Abdul Nasser Farawneh, mkuu wa Idara ya Utafiti katika Kamati ya Masuala ya Mateka na Wafungwa wa Zamani wa Palestina, hivi sasa kuna Wapalestina 5,800 wanaoshikiliwa katika jela za utawala wa Kizayuni wa Israel na miongoni mwao kuna wanawake 62 na watoto 200. Aidha miongoni mwa mateka hao Wapalestina kuna wagonjwa 700.
Hivi sasa kufuatia kuenea ugonjwa hatari wa corona katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu yaani Israel, kadhia ya kufariki mateka Wapalestina inajadiliwa kwa kina na wanamapambano wa kupigania ukombozi wa Palestina.