Ndege za kivita za utawala wa Kizayuni zashambulia Ukanda wa Ghaza
Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limeetekeleza mashambulizi katika Ukanda wa Gaza usiku wa kuamkia leo Jumamosi.
Vyombo vya habari vya Palestina vimesema bado haijaweza kubainika kuhusu maafa yoyote yaliyojiri baada ya hujuma hiyo.
Mashambulizi hayo yamejiri masaa mawili baada ya vyombo vya habari kutangaza kuwa maroketi mawili yamevurumishwa kutoka Ukanda wa Ghaza kuelekea vitongoji vya walowezi wa Kizayuni karibu na ukanda huo.
Hapo kabla, Abu Ubaida, Msemaji wa Brigedi za Ezzedin Qassam, Tawi la Kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, alitangaza kuwa makundi ya muqawama na kupigania ukombozi wa Paletina yataufanya utawala wa Kizayuni ujute kukalia kwa mabavu maeneo zaidi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Abu Ubaida ametoa tamko hilo baada ya wakuu wa Marekani kutangaza kuwa Rais Donald Trump anatazamiwa kuzindua mpango mpya kuhusu Palestina.
Watawala wakuu wa Israel, waziri mkuu Benjamin Netanyahu, kiongozi wa chama cha Likud na Benny Gantz kiongozi wa chama cha Blu na Nyeupe, walifikia makubaliano ya kutwaa asilimia 30 ya eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi na kuliunganisha na ardhi nyingine zilizoghusubiwa za Palestina ifikapo mwezi Julai mwaka huu wa 2020. Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kuwadia muda wa kutekelezwa mpango huo, mashinikizo dhidi ya utawala wa Israel yanaonekana kushadidi kila upande.
Mpango wa utawala haramu wa Israel wa kutwaa asilimia 30 ya eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi na kuliunganisha na ardhi nyingine zilizoghusubiwa za Palestina ni miongoni mwa vipengee muhimu vya mpango wa kibaguzi wa “Muamala wa Karne” uliozinduliwa mwezi Januari na Rais Trump wa Marekani.