Maafisa 2 wa UN huko Israel wasimamishwa kazi kwa ufuska
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i61996-maafisa_2_wa_un_huko_israel_wasimamishwa_kazi_kwa_ufuska
Umoja wa Mataifa umewasimamisha kazi maafisa wake wawili wa timu ya operesheni za usalama eneo la Asia Magharibi baada ya kubainika kuwa walijihusisha na vitendo vya ufuska ndani ya utawala haramu wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 04, 2020 03:39 UTC
  • Maafisa 2 wa UN huko Israel wasimamishwa kazi kwa ufuska

Umoja wa Mataifa umewasimamisha kazi maafisa wake wawili wa timu ya operesheni za usalama eneo la Asia Magharibi baada ya kubainika kuwa walijihusisha na vitendo vya ufuska ndani ya utawala haramu wa Israel.

Ofisi ya Kutathmini Masuala ya Ndani ya Umoja wa Mataifa baada ya uchunguzi wa awali imewapata na hatia wawili hao kwa kujihusisha na ufuska na imewasimamisha kazi kwa muda bila mshahara.

Stéphane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema katika taarifa kuwa, maafisa hao wawili wa UN walinaswa kwenye kanda ya video wakifanya vitendo hivyo vichafu ndani ya gari la umoja huo mjini Tel Aviv.

Amesema hatima ya maafisa hao waliorekodiwa wakimdhalilisha kingono mwanamke aliyekuwa amevalia vazi la rangi nyekundu itajulikana baada ya kukamilika uchunguzi wa kina.

Visa vya askari na maafisa wa Umoja wa Mataifa kujihusisha na ubakaji, udhalilishaji na vitendo vingine viovu katika nchi mbalimbali duniani vimeongezeka katika miaka ya hivi karibuni.

Askari wa kulinda amani wa UN nchini Mali

Mwaka 2019, kuliripotiwa madai 175  ya ubakaji na kunajisiwa wanawake na watoto wadogo na askari na maafisa wa Umoja wa Mataifa katika nchi tofauti duniani.

Aidha mwaka 2018, wanajeshi 46 wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) raia wa Ghana walirejeshwa nyumbani kutoka kaskazini magharibi mwa Sudan Kusini, baada ya kukabiliwa na tuhuma za ubakaji.