Maelfu ya Waisraeli waandamana mkabala wa makazi ya Netanyahu wakitaka ajiuzulu
Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni jana usiku vilitangaza habari ya kuendelea maandamano ya maelfu ya wakazi wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu mkabala na makazi ya Waziri Mkuu wa utawala huo unaoikalia Quds Tukufu kwa mabavu.
Tovuti ya habari ya Times Israel imeripoti kuwa, wafanya maandamano wanatazamia leo kuendelea na manadamano yao dhidi ya Netanyahu. Wakazi wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu wamekuwa wakifanya maandamano kupinga siasa za Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni kwa zaidi ya wiki mbili sasa.
Maandamano hayo sasa yameenea hadi karibu na makazi ya Waziri Mkuu huyo wa Israel katika mtaa wa Balfour. Waandamanaji wamekosoa utendaji dhaifu wa serikali ya Netanyahu katika kudhibiti maambukizi ya corona na kesi za ufisadi wa fedha zinazomkabili yeye na mkewe na kutaka ajiuzulu haraka iwezekanavyo.
Netanyahu katika muda wa miezi ya karibuni amekabiliwa na kesi nne za ufisadi wa fedha; mafaili ambayo yametajwa na vyombo vya habari kwa majina ya faili la 1000, faili la 2000, faili la 3000 na faili la 4000.