Athari mbaya za mlipuko wa Beirut
Mlipuko mkubwa uliotokea Jumanne wiki hii mjini Beirut nchini Lebanon ambao vyombo vya habari vimeufananisha na mashambulizi ya mabomu ya nyuklia yaliyofanywa na Marekani dhidi ya mji wa Hiroshima nchini Japan wakati wa vita vya Pili vya Dunia, mbali na sababu za kutokea kwake, una taathira muhimu kwa nchi ndogo na muhimu ya Lebanon.
Hadi sasa sababu na nani amehusika na mlipuko huo mkubwa uliotokea kwenye bandari ya Beirut bado haijajulikana vyema. Je umetokana na uzembe wa maafisa husika au la? Je ni shambulizi na hujuma ya adui? Je tukio hilo linahusiana na pande za ndani ya nchi au nje ya Lebanon au la? Pamoja na hayo yote mlipuko huo utakuwa na taathira kubwa na nzito mno kwa Lebanon.
Taarifa iliyotolewa na harakati ya Hizbullah ya Lebanon imesema kuwa: "Maafa haya makubwa na yenye uharibifu mkubwa, na taathira zake hatari katika nyanja mbalimbali za kibinadamu, kiafya, kijamii na kiuchumi yanazidisha udharura wa kuwepo mshikamano na umoja kati ya Walebanoni wote na makundi yote ya kisiasa, na kuchukuliwa hatua ya pamoja ya kuvuka salama kipindi hiki chenye maumivu makubwa."
Athari mbaya ya kwanza kabisa ya mlipuko wa Beirut ni hasara zake kubwa za roho za watu walioaga dunia katika tukio hilo. Takwimu zinaonyesha kuwa hadi sasa watu wasiopungua mia moja wamefariki dunia katika mlipuko huo na wengine zaidi ya elfu nne wamejeruhiwa. Kiwango hiki kikubwa cha majeruhi kinazidisha uwezekano wa kuongezeka idadi ya watu walioaga dunia kutokana na mlipuko huo. Mbali na kupoteza nguvu kazi muhimu katika mlipuko huo wa Beirut, tukio hilo pia litakuwa na athari mbaya sana za kiroho kwa raia wa Lebanon. Hii ni kutokana na kupoteza ndugu na raia wenzao na pia uharibifu mkubwa uliosababishwa na mlipuko huo.

Athari ya pili mbaya na kubwa ya mlipuko wa bandari ya Beirut ambao umekumbusha mashambulizi ya silaha ndogo ya nyuklia, inaonekana katika medani ya uchumi. Baadhi ya vyombo vya habari vya Lebanon vimeripoti kuwa, mrengo unaoungwa mkono na nchi za Magharibi nchini humo umehamishia nje ya nchi kiwango kikubwa cha fedha kinachokadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 20 katika kipindi kifupi; suala ambalo limepelekea kuanguka thamani ya sarafu ya taifa ya Lebanon kwa asilimia 70. Mlipuko wa bandari ya Beirut unazidisha matatizo ya kiuchumi ya Walebanoni na serikali ya Hassan Diab.
Gazeti la The Guardian la Uingereza limeandika kuwa: “Asilmia 90 ya ngano inayotumiwa nchini Lebanon inatoka nje ya nchi hiyo na sehemu kubwa ya ngano hiyo ilikuwa ikiingizwa nchini kupitia sehemu iliyoharibiwa ya bandari ya Beirut. Hii ni pamoja na kuwa katika kipindi cha miezi kadha iliyopita, bei ya bidhaa za chakula nchini Lebanon zimepanda kwa asilimia 80.”
Nalo gazeti la al Akhbar la Lebanon limeandika kuwa: “Bidhaa zinazoingizwa katika bandari ya Beirut ni zaidi ya asilimia 70 ya bidhaa zote zinazoingizwa nchini Lebanon kutoka nje ya nchi.”
Kuhusu athari mbaya za mlipuko wa bandari ya Beirut, balozi wa zamani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Lebanon Ahmad Dastmalchian anasema: Mlipuko huu umesababisha hasara kubwa sana kwa akiba ya ngano ya Lebanon na yumkini asilimia 90 ya akiba ya ngano iliyokuwa bandarini hapo imeharibiwa. Suala hili peke yake linaweza kusababisha matatizo makubwa kwa maisha ya raia wa nchi hiyo, na serikali haina budi kutilia maanani kadhia hii.”

Mbali na hayo ujenzi na ukarabati wa nyumba, majengo, maeneo ya kibiashara na bandari yenyewe ya Beiruti unahitaji kiwango kikubwa cha fedha ambacho ni mzigo mzito sana kwa uchumi wa sasa wa Lebanon.
Mlipuko wa Beirut pia umekuwa na taathira mbaya katika uwanja wa kisiasa wa nchi hiyo. Serikali ya sasa ya Lebanon haihusiki na mlipuko huo na inaonekana kuwa hata haikufanya uzembe wa aina yoyote katika tukio hilo. Hata hivyo mlipuko huo utazidisha mashinikizo ya kisiasa kwa serikali ya Waziri Mkuu, Hassan Diab.
Serikali hiyo imekuwa chini ya mashinikizo makubwa zaidi ya kisiasa katika kipindi cha miezi sita ya umri wake, na wapinzani wake wa ndani na nje ya nchi wanafanya jitihada kubwa za kuhakikisha inaondoka madarakani. Mashinikizo ya hivi karibuni zaidi ni kujiuzulu kwa aliyekuwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Lebanon, Nassif Hitti, jumatatu ya wiki hii.
Sasa wapinzani wa serikali ya Beirut watatumia vibaya hisia na matatizo ya kiroho ya wananchi kwa ajili ya kuzidisha vita vya kinafsi dhidi ya serikali ya Hassan Diab.