Taathira za kiusalama za ‘makubaliano ya usaliti’ ya Israel na Imarati
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i62859-taathira_za_kiusalama_za_makubaliano_ya_usaliti’_ya_israel_na_imarati
Makubaliano ya hiana na usaliti ya Imarati na utawala dhalimu wa Israel ya kuanzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia baina yao yatakuwa na matokeo na taathira tofauti katika uga wa usalama.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 17, 2020 02:08 UTC
  • Taathira za kiusalama za ‘makubaliano ya usaliti’ ya Israel na Imarati

Makubaliano ya hiana na usaliti ya Imarati na utawala dhalimu wa Israel ya kuanzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia baina yao yatakuwa na matokeo na taathira tofauti katika uga wa usalama.

Kabla ya hapo Israel na Imarati zilikuwa na uhusiano katika nyuga mbalimbali na hata gazeti la Israel Hayom lilitangaza kuwa, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel katika kipindi cha miaka miwili iliyopita alifanya safari mbili za siri huko Abu Dhabi.

Pamoja na hayo uhusiano huo haukuwa na taathira kwa usalama wa eneo la Asia Magharibi. Hii ni katika hali ambayo, kutangazwa wazi uhusiano huo kutakuwa na taathira kwa usalama wa pande mbili na Ukanda mzima wa Asia Magharibi.

Moja ya taathira za kiusalama za makubaliano hayo ya hiana ni kwamba,  Imarati ambayo inafuatilia suala la kugeuka na kuwa kigezo cha ustawi wa kiuchumi katika eneo hili, itakabiliwa na ukosefu wa usalama. Hii ni katika hali ambayo, sharti kuu na muhimu la ustawi wa kiuchumi ni kuwa na usalama imara.

Viongozi wa Marekani, Imarati na Israel waliotangaza kufikiwa makubaliano ya Israel na Imarati ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia

Ubalozi wa Imarati nchini Libya umechomwa moto saa 72 tu baada ya kutangazwa makubaliano hayo. Wananchi wa Libya wenye hasira wamechoma moto jengo la ubalozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli wakilalamikia hatua ya serikali ya Abu Dhabi ya kufikia makubaliano ya kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala dhalimu wa Israel. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kuna uwezekano wa kukaririwa tukio kama hilo dhidi ya balozi zake nyingine za Imarati zilizoko katika mataifa mbalimbali.

Imarati ni moja ya wanachama wakuu wa muungano vamizi wa kijeshi nchini Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia. Baada ya kuongezeka harakati za kijeshi za Abu Dhabi dhidi ya Yemen, mwaka uliopita nchi hiyo ilishuhudia milipuko ya meli za mafuta katika Bandari ya al Fujairah na vilevile hatua za jeshi na kamati za kujitolea za wananchi dhidi ya Imarati ambazo ziliulenga usalama wa nchi hiyo na kuzusha wasiwasi mkubwa kwa watawala wa nchi hiyo sambamba na kushadididi hitilafu za ndani. Matokeo yake, Imarati ililazimika kuchukua uamuzi wa kuyaondoa majeshi yake nchini Yemen na kupunguza ushiriki wake katika vita hivyo. 

Utawala wa Kizayuni wa Israel unachukiwa mno katika Ulimwengu wa Kiislamu kiasi kwamba, kufikia makubaliano na utawala huo kwa ajili ya kuanzisha uhusiano rasmi kunaweza kuwa na matokeo hasi ya ndani na hata kupelekea kuibuka hitilafu ndani ya utawala wa Abu Dhabi.

Maandamano ya kupinga makubaliano ya Israel na Imarati ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia

Moja ya sababu ya jambo hilo ni kuwa, makubaliano ya Imarati na Israel yamefikiwa katika mazingira ambayo Tel Aviv ikipata himaya na uungaji mkono wa Marekani imeshadidisha vitendo vyake vya utumiaji mabavu dhidi ya Wapalestina; na kwa muktadha huo, makubaliano hayo maana yake ni kuunga mkono hiana, usaliti  na jinai za Israel dhidi ya wananchi wa Palestina..

Moja ya upande mwingine wa kiusalama wa makubaliano ya usaliti ni jibu la makundi ya mapambano ya Kiislamu ya Palestina. Makubaliano haya ya usaliti  hayana chochote kwa Wapalestina kinyume na mapatano ya Camp David ya 1978 na makubaliano ya Wadi Araba ya 1974 ambayo yalidaiwa kuwa ya amani mkabala na ardhi, yaani Wapalestina walitakiwa kupewa baadhi ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel mkabala wa mapatano hayo. Mapatano haya mkabala na sifuri yana ujumbe muhimu kwa Wapalestina nao.

Ubalozi wa Imarati mjini Tripoli umeshambuliwa na kuchomwa moto na wananchi wenye hasira wanaopinga makubaliano ya Tel Aviv na Abu Dhabi

Ukweli wa mambo ni kuwa, kupitia makubaliano haya Wapalestina wamediriki na kufikia natija hii kwamba, wakiwa na lengo la kujilinda katu hawapaswi kuzitegemea nchi za Kiarabu kwa kuwa ni Waarabu wenzao, kwani kuna uwezekano wa kuongezeka nchi za Kiarabu ambazo zitaanzisha uhusiano rasmi na utawala huo ghasibu.

Kuhusiana na hilo, Khalil al-Hayya, mjumbe wa Idara ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kuwa, makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina ya watawala wa Imarati na adui Israel yanatoa pigo kwa umoja wa Waarabu. Ameongeza kuwa, kuna harakati zinafanyika baina ya makundi ya Palestina ndani na nje kwa ajili ya kufikia makubaliano ya kuongeza harakati za kukabiliana na mwenendo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel na mpango wa kumega ardhi ya Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan na kuziunganisha na ardhi nyingine zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.