Waziri wa Mambo ya Nje wa Yemen: Arab League imepoteza mwelekeo
(last modified Wed, 26 Aug 2020 08:14:46 GMT )
Aug 26, 2020 08:14 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Yemen: Arab League imepoteza mwelekeo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema kuwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) haina uwezo wa kulinda maslahi ya nchi za Kiarabu mbele ya njama mbalimbali zinaofanywa na utawala haramu wa Israel na washirika wake.

Hisham Sharaf Abdullah ameitaja hali ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuwa ni "mahatuti" na kuongeza kuwa, hali hiyo itapelekea kusambaratika kikamilifu jumuiya hiyo. 

Hisham Sharaf Abdullah amekosoa msimamo wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusiana na uvamizi wa Saudi Arabia dhidi ya ardhi ya Yemen na amezitaka nchi wanachama katika jumuiya hiyo zizuiye kusambaratika kwake. 

Awali Majid al Fityani ambaye ni afisa wa ngazi za juu wa Baraza la Mapinduzi la harakati ya Fat'h ya Palestina alikuwa amekosoa msimamo wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusiana na hatua ya Imarati ya kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel. 

Jumuiya hiyo inakosolewa sana na nchi wanachama kutokana na kufuata misimamo ya Saudi Arabia na washirika wake na kufumbia jicho maslahi ya nchi wanachama hususan zile zinazopinga siasa za kibeberu za Marekani na mwanaharamu wake, Israel.