Bin Salman aonana kwa siri ya ujumbe wa utawala wa Kizayuni
Afisa mmoja wa shirika la kijasusi la Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) ametangaza habari ya kufanyika mazungumzo ya siri baina ya mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman na ujumbe mmoja wa utawala wa Kizayuni.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Mehr, afisa huyo wa kijasusi wa Imarati ambaye hakutaka jina lake litajwe ametangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, mazungumzo ya siri baina ya Muhammad bin Salman na ujumbe wa utawala wa Kizayuni, yamefanyika katika meli moja ya anasa ya Bin Salman kwenye Bahari ya Sham (Redi Sea) na kuhudhuriwa pia na mkuu wa mashirika ya kijasusi ya Saudi Arabia.
Habari nyingine inasema kuwa, Muhammad Abdul Salam, Msemaji wa Harakati ya Answarullah ya Yemen ameonya kwamba, tawala wa kiimla za Kiarabu ambazo zinapigana vikumbo katika kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni haziwezi kubadilisha ukweli wa mambo kwani huko nyuma pia tawala hizo za kidikteta zilikuwa na uhusiano na ushirikiano mkubwa wa siri na Wazayuni.
Katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, limezuka wimbi la tawala za kidikteta za Kiarabu kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni.
Njama zinazofanywa na tawala hizo kupitia kutangaza rasmi uhusiano wao na utawala katili wa Israel zinafanyika katika hali ambayo kwa miaka mingi utawala huo ghasibu umekuwa ukifanya jinai kubwa dhidi ya Wapalestina na unaendelea kuyakalia kwa mabavu maeneo ya Waarabu na ya Waislamu.