Wananchi wengi wa nchi za Kiarabu hawataki uhusiano na Wazayuni
Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa katika nchi zaidi ya 10 za Kiarabu unaonesha kuwa sehemu kubwa kupindukia ya wananchi wa nchi hizo hawataki uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Shirika la habari la Shahab la Palestina limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na Kituo cha Kiarabu cha Uchunguzi na Utafiti wa Kisiasa yanaonesha kuwa asilimia 88 ya wananchi wa nchi za Kiarabu wanapinga kutambuliwa ramsi Israel na nchi zao.
Walioshiriki kwenye uchunguzi huo wa maoni wametoa sababu mbalimbali zikiwemo siasa za ubaguzi wa rangi za utawala wa Kizayuni na kuendelea kwake kuyakalia kwa mabavu maeneo ya Wapalestina na ya Waarabu.
Zaidi ya asilimia 80 ya walioshiriki kwenye uchunguzi huo wa maoni wanasema, siasa za Marekani na vitisho vya madola ya kibeberu yanayouunga mkono utawala wa Kizayuni dhidi ya usalama na amani ya eneo hili ni sababu nyingine iliyowafanya wananchi wengi sana wa nchi za Kiarabu kupinga kutambuliwa rasmi utawala wa Kizayuni wa Israel na nchi zao.
Uchunguzi huo wa maoni umefanyika katika nchi 13 za Kiarabu ambazo ni Morocco, Mauritania, Algeria, Tunisia, Misri, Sudan, Palestina, Lebanon, Jordan, Iraq, Saudi Arabia, Kuwait, na Qatar. Watu 28 elfu wameshiriki kwenye uchunguzi huo wa maoni.
Baada ya nchi mbili za Imarati na Bahrain kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni, tarehe 15 Septemba mwaka huu zilijipeleka mbele ya rais wa Marekani, Donald Trump kwenda kutia saini makubaliano rasmi baina ya nchi zao na utawala ghasibu wa Kizayuni. Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni naye alishiriki kwenye utiaji saini wa makubaliano hayo.