Oct 08, 2020 07:32 UTC
  • Milioni ya Wairaq wafanya ziara ya Arubaini kuwawakisha Waislamu wenzao duniani

Milioni ya Wairaq wamewasili katika Haram ya Imam Husain AS huko Karbala kuwawakilisha mamilioni ya wapenzi wa Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume Muhammad SAW ambao mwaka huu wameshindwa kwenda Iraq kushiriki kumbukumbu hizo kutokana na corona.

Baada ya kutembea kwa miguu kwa mamia ya kilomita, kundi la mwisho la maashiki wa Imam Husain AS liliwasili Karbala jana Jumatano kwa ajili ya maadhimisho yaliyofana ya 40 ya Imam Husain AS.

Kama tunavyojua, idadi kubwa ya Waislamu na wafuasi wa dini nyinginezo kwa miaka mingi huwa wanatembea kwa miguu ambako ni maarufu kwa jina la Mashaya, kutoka mji wa Najaf kwa ajili ya kwenda kufanya ziara katika Haram na bwana huyo wa mashahidi huko Karbala katika maadhimisho ya 40 ya Imam Husain AS.

Takwimu rasmi zinaonesha kuwa, mwaka jana zaidi ya wafanya ziara milioni 18 walishiriki katika matembezi hayo ya Arubaini ya Imam Husain AS, matembezi ambayo yanahesabiwa kuwa ni mjumuiko mkubwa zaidi wa kidini wa kila mwaka duniani. Taarifa zinasema kuwa, wafanya ziara kutoka nchi 80 duniani hushiriki katika matembezi hayo ya kimaanawi yanayoshirikisha wazee kwa vijana, wanawake kwa wanaume, wakubwa kwa wadogo.

Arubaini ya Imam Husain AS nchini Pakistan

 

Mwaka huu matembezi hayo yamefanywa na mamilioni ya maashiki wa Imam Husain AS wa kona zote za Iraq tu bila ya kushirikisha wafanya ziara kutoka nje ya nchi hiyo kutokana na maambukizi ya kirusi cha corona. 

Wapenzi wa Ahlul Bayt AS hapa nchini Iran ambao mara hii haikuyumkinika kwao kushiriki kwenye matembezi ya Arubaini ya Imam Husain AS huko Iraq, leo Alkhamisi wanashiriki katika kumbukumbu hizi wakiwa majumbani mwao, kwa kusoma Ziara ya Arubaini ya mtukufu huyo na kujiunga na maashiki wenzao wa watu wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW kote duniani na hasa huko Karbala Iraq.

Tags