HAMAS: Chokochoko za Ufaransa zimeumiza hisia za Waislamu duniani
(last modified Mon, 26 Oct 2020 11:44:00 GMT )
Oct 26, 2020 11:44 UTC
  • HAMAS: Chokochoko za Ufaransa zimeumiza hisia za Waislamu duniani

Afisa mmoja wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema hatua za kichochezi na kichokozi za maafisa wa serikali ya Ufaransa za kuunga mkono kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW na matukufu ya Kiislamu zimeumiza hisia na nyoyo za Waislamu kote duniani.

Sami Abu Zuhri, msemaji mwandamizi wa HAMAS amesema: Hatua ya (Rais wa Ufaransa Emmanuel) Macron ya kushajiisha kuchapishwa vibonzo vya kumtusi na kumvunjia heshima Mtume Muhammad (SAW) ni jitihada za kuhuisha vita vya kidini, ambavyo Ufaransa ilikuwa chimbuko na muasisi wake.

Amesema kuchapisha katuni za kumkejeli Mtume Mtukufu, kumechochea hisia za umma wa Kiislamu, na ni hujuma kwa Uislamu na itikadi zake.  

Jarida la Kifaransa la Charlie Hebdo siku kadhaa zilizopita lilichapisha tena kibonzo kinachomtusi na kumvunjia heshima Mtume Muhammad (SAW). 

Waislamu kote duniani wametoa mwito wa kususiwa bidhaa za Ufaransa

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alitetea kitendo hicho kiovu kwa kisingizio kuwa nchi hiyo inaheshimu uhuru wa kujieleza. Amesema katika ujumbe wa Twitter kuwa: Hakuna kitu kitakachotufanya tusalimu amri.

Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Morocco sambamba na kulaani hatua hiyo ya kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad (SAW), imesema kisingizio cha uhuru wa kujieleza hakiwezi kuhalalisha vitendo hivyo vya kichokozi na kuutukana Uislamu na matukufu yake.

Tags