Sheria mpya ya uchaguzi Iraq; namna ilivyotungwa na jinsi ilivyopokewa
(last modified Mon, 09 Nov 2020 02:32:26 GMT )
Nov 09, 2020 02:32 UTC
  • Sheria mpya ya uchaguzi Iraq; namna ilivyotungwa na jinsi ilivyopokewa

Sheria mpya ya uchaguzi ya Iraq imesainiwa na rais Barham Salih baada ya kupitishwa na bunge la nchi hiyo.

Oktoba mwaka jana, Iraq ilishuhudia maandamano ya wananchi yaliyopelekea kujiuzulu aliyekuwa waziri mkuu wakati huo Adil Abdul-Mahdi mnamo tarehe mosi Desemba. Baada ya kujiuzulu Abdul-Mahdi, moja ya hatua zilizochukuliwa na bunge katika mwezi huohuo wa Desemba ilikuwa ni kupasisha sheria mpya ya uchaguzi, ambayo ilipingwa na baadhi ya mirengo ya kisiasa ya nchi hiyo. Sababu kuu ya kupingwa sheria hiyo mpya ilikuwa ni juu ya mgawanyo wa majimbo ya ubunge. 

Adil Abdul-Mahdi

Baada ya kupita takriban miezi 10, mnamo tarehe 10 Oktoba mwaka huu bunge la Iraq lilipasisha sheria nyingine mpya ya uchaguzi. Kwa mujibu wa sheria hiyo, mikoa ya Iraq imegawanywa katika majimbo kadhaa ya uchaguzi yanayozingatia pia nafasi za wanawake. Katika sheria hiyo mpya, majimbo ya uchaguzi katika mikoa yote ya Iraq yatakuwa ni 83, ambapo majimbo 17 ni kwa ajili ya eneo la Baghdad, manane Nainawa, sita eneo la Basra, matano kwa ajili ya maeneo ya Dhi Qar na Sulaymaniyah, manne katika kila moja kati ya mikoa minne ya Babil, Al Anbar, Erbil na Diyala, matatu kwa kila moja kati ya mikoa ya Kirkuk, Najaf al Ashraf, Salahuddin, Duhok, Diwaniya, Karbala, Wasit na Maysan na mawili kwa ajili ya mkoa wa al Muthanna.

Kwa kuzingatia kwamba, idadi ya majimbo ya uchaguzi katika kila mkoa inatakiwa ilingane na nafasi maalumu za wanawake, ndiyo kusema kuwa katika bunge lijalo la Iraq nafasi 83 zitatengwa kwa ajili ya wanawake. Baada ya Rais Barham Salih kusaini sheria hiyo mpya ya uchaguzi alisema: "sheria hii haiakisi mambo yote tunayoyataka; lakini ni hatua moja ya mabadiliko kwa ajili ya hali bora na pia ni jiwe la msingi la mageuzi."

Wabunge wa Iraq wakipiga kura

Sheria mpya ya uchaguzi ya Iraq inatafautiana katika mambo kadhaa na sheria iliyokuwa ikitumika tangu mwaka 2005 hadi sasa. Kwanza ni kwamba, katika sheria hiyo mpya, wagombea watakuwa wakijiandikisha katika uchaguzi kama watu binafsi; wakati hapo kabla wananchi walikuwa wakiwapigia kura wagombea walioteuliwa na vyama. Pili ni kwamba, katika chaguzi za bunge zilizofanyika nchini Iraq kuanzia mwaka 2005 hadi 2018 kila mkoa ulikuwa ukihesabiwa kuwa jimbo la uchaguzi, lakini sheria mpya ya sasa imeigawa mikoa yote 18 ya Iraq katika majimbo madogo zaidi ya uchaguzi.

Hivi sasa ambapo imesalia miezi saba hadi kufanyika uchaguzi wa mapema wa bunge la Iraq, utekelezaji wa sheria mpya ya uchaguzi unakabiliwa na changamoto kadhaa. Changamoto muhimu zaidi ni kwamba, bunge la Iraq lina wabunge 329, lakini ni wabunge 183 tu ndio waliohudhuria kikao cha bunge wakati wa kuipigia kura sheria hiyo mpya ya uchaguzi. Mbunge wa Iraq Hassan Khalat'i anasema: "bunge lilifanya kikao chake cha kawaida kukiwepo wabunge 183 ili kukamilisha upitishaji wa sheria mpya ya uchaguzi; na shera hiyo ikapitishwa kwa kura 105 kati ya wabunge wote waliohudhuria." Kwa maneno mengine ni kwamba, hata kama sheria mpya ya uchaguzi imepitishwa kwa wingi wa kura za wabunge waliokuwepo bungeni lakini wabunge 146 hawakuhudhuria kikao hicho cha kuipigia kura sheria hiyo mpya ya uchaguzi.

Sababu moja iliyoyafanya makundi na mirengo kadhaa ya Iraq ipinge sheria mpya ya uchaguzi ni kwamba, kwa mtazamo wa makundi hayo, sheria hiyo itapunguza idadi ya viti vyao bungeni. Kwa mfano Wakurdi wanaamini kuwa, kugawanywa majimbo katika maeneo yanayozozaniwa kutawafanya wapoteze kura zao hususan katika maeneo yenye mizozo ambayo idadi kubwa ya wakazi wake ni Waarabu na Waturkaman.

Rais Barham Salih

Kutokana na yote hayo tunaweza kusema kwamba, hata kama sheria mpya ya uchaguzi imepitishwa katika bunge la Iraq na kusainiwa na rais Barhma Salih, lakini kutokana na upinzani mkubwa uliopo, kuna shaka kubwa kama sheria hiyo itaweza kutekelezwa katika uchaguzi ujao wa bunge uliopangwa kufanyika Juni 2021.../