Arab League yataka kuokolewa mateka wa Kipalestina katika jela za Israel
Kufuatia kufa shahidi mateka Mpalestina Kamal Abu Waar akiwa katika jela ya utawala wa Kizayuni wa Israel, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imetoa mwito wa kuchukiliwa hatua za dharura za kuwanusuru mateka wengine wa Kipalestina wanaozuiliwa katika mazingira ya kuogofya katika jela na korokoro hizo za Wazayuni.
Taarifa iliyotolewa jana Jumatano na Arab League mbali na kulaani kufa shahidi mateka huyo Mpalestina ambaye kwa muda mrefu sana amekuwa akiugua saratani, imeyataka mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu kutekeleza wajibu wao wa kuhakikisha kuwa sheria za kulindwa mateka wa Kipalestina katika jela hizo za Wazayuni zinatekelezwa.
Saeed Abu Ali, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ameeleza bayana kuwa, "kufa shahidi Kamal Abu Waar, mateka wa Kipalestina aliyekuwa na saratani na virusi vya corona, kutokana na kunyimwa matibabu na utawala wa Kizayuni akiwa kizuizini, ni jinai mpya iliyojumuishwa kwenye faili jeusi la jinai za Israel."
Kwa mujibu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), kufa shahidi Kamal Abu Waar kumepelekea idadi ya wafungwa waliokufa shahidi kufika 226 na kwamba hii ni dalili ya wazi kuwa jinai za kivita za utawala wa Kizayuni dhidi ya wafungwa Wapalestina zingali zinaendelea.

Karibu mateka 4,800 wa Palestina wakiwemo wanawake 41 na watoto 140 wanashikiliwa katika jela za kuogofya za utawala wa Kizayuni wa Israel.
Mateka hao wa Palestina ni kati ya waathirika wakubwa wa jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel. Inakadiriwa kuwa tokea mwaka 1967, Wapalestina 226 wamekufa shahidi katika jela za utawala wa Kizayuni wa Israel.